20 February 2013



Hofu ya Al Qaeda Ukerewe



*Wananchi wakihusisha chuo na ugaidi
*Mbunge ataharuki, aandaa hoja binafsi
*Mkuu wa Mkoa, DC wakwepa kunena

HOFU ya kuwapo kwa magaidi wa mtandao wa Al- Qaeda, imetanda katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, baada ya kuvuja kwa taarifa za kuanzishwa kwa chuo kimoja cha kidini kinachohofiwa kutoa mafunzo yenye mwelekeo wa kigaidi visiwani humo.

Taarifa hizo zimeeleza kuwa chuo hicho kinajulikana kwa jina la Markaz, Aljazeera na kimeanzishwa kwa ufadhili wa raia wa kigeni ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu.

Makundi yanayotajwa kufadhili uendeshaji wa chuo hicho ni Al-Qaeda na Al shabab yanayoaminika kuwa na mtandao mkubwa wa ugaidi duniani.

Uchunguzi uliofanywa na Mtanzania Jumatano wilayani Ukerewe, umebaini kuwa chuo cha Markaz kinatoa mafunzo kwa watu wa rika mbalimbali yenye mwelekeo wa kujihami na kushambulia kama Karate na Kung-fu.

Aidha, taarifa nyingine za kiuchunguzi ambazo gazeti hili lilidokezwa na wakazi wa kisiwani humo walioonyesha wasiwasi wa kuwepo kwa chuo hicho, zilidai kuwa, aina nyingine ya mafunzo yanayotolewa katika chuo hicho na kushambuliana kwa silaha aina ya jambia.

Uchunguzi ulibaini zaidi kuwa, wanafunzi katika chuo hicho ni watoto wenye umri wa kati ya miaka saba hadi 10 na pia kuna wanafunzi vijana na watu wazima.

Baadhi ya wakazi wa wilayani humo waliopata kufanya kazi katika chuo hicho, waliliambia gazeti hili kuwa chuo hicho kimekuwa kikipokea mizigo ya aina mbalimbali, ikiwa imefungwa kwenye maboksi ambayo katika udadisi wao walibaini kuwa, baadhi ya bidhaa zinazokuwa kwenye shehena hizo ni kanzu, seti za televisheni, vitabu na silaha za aina mbalimbali.

Walidai kuwa, walianza kukitilia mashaka chuo hicho baada ya kubaini kinapokea silaha katika baadhi ya mizigo yake.

Mbali ya hilo, wakazi hao walilieleza gazeti hili kwamba aina ya wageni wanaoingia na kutoka visiwani humo kwa minajili ya kukitembelea chuo hicho, ni jambo jingine ambalo limekuwa likiwafanya wazidi kukitilia shaka chuo hicho. 

Kwa mujibu wa wakazi hao, wageni hao wamekuwa wakiingia kisiwani kwa njia ya mitumbwi wakipita katika njia za panya nyakati za usiku.

Wageni hao kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo la Nansio ni wale wanaodaiwa na kuaminika kutoka katika nchi jirani za Kenya na Uganda ambazo mipaka ya ziwa Victoria inapita.

Wafanyabiashara wanaojihusisha na usafirishaji abiria waliozungumza na gazeti la Mtanzania Jumatano walieleza kuwa, wageni wanaowapakia kuwapeleka chuo cha Markaz au maeneo mengine ya kisiwa hicho huwalazimisha kuondoa misalaba waliyoivaa shingoni au waliyotundika katika magari na pia huwataka wazime redio katika magari yao.

Hofu hiyo ya wakazi wa Nansio ilisababisha gazeti hili kumtafuta Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli (Chadema) ambaye naye alikiri kulifahamu jambo hilo.

Akizungumza kupitia simu yake ya kiganjani, Machemli alisema chuo hicho kinatoa mafunzo ambayo wakazi wake wanayahusisha na matendo ya kigaidi.

Mbunge huyo alisema hofu zaidi kuhusu chuo hicho ni kuwapo kwa taarifa zinazodai kwamba, baadhi ya wanachuo ambao wamewahi kupata mafunzo chuoni wanatajwa kuwa wanachama wa makundi ya kigaidi ya Al Qaeda na Al-Shabab.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, miongoni mwa hatua ambazo amepata kuzichukua ili kutafuta majibu ya wasiwasi wa wananchi wa Ukerewe ni pamoja na kumsaka mmoja wa watu anayekijua chuo hicho.

“Ni kweli tuna wasiwasi na hatuoni kazi ya umma kinachojihusisha nacho. Niliwahi kumuuliza Diwani wa Kata ya Nansio, Sheikh Ramadhani Mazige (CCM) kuhusu uhalali wa kuwapo kwa chuo hicho kwa sababu alikuwa akisimamia ujenzi wake na nikashauri juu ya umuhimu wa kubadili aina ya mafunzo yanayofundishwa chuoni hapo na jibu lake lilikuwa wenye chuo hawataki.

Alipoulizwa iwapo anawafahamu wamiliki wa chuo hicho, alikana kuwatambua kwa kueleza kuwa, jitihada zake za kuwafahamu hazikufanikiwa baada ya Diwani Mazege kukataa kuwataja.

Machemli alisema kuwa, amepanga kulifikisha suala hilo kama hoja binafsi kwenye Baraza la Madiwani ili kuomba kibali cha kutembelea chuo hicho kuona shughuli zinazofanyika na kwamba iwapo atakwamishwa, atalifikisha suala hilo katika ngazi za juu.

Akizungumza kuhusu raia wa kigeni wanaopitia njia za panya kwa usafiri wa mitumbwi nyakati za usiku kufika chuoni hapo, Machemli alisema hilo hawezi kulipinga.

Kwa mujibu wa Machemli, jiografia ya visiwa vya Ukerewe inavifanya viwe wazi kuhusu mipaka yake na kwamba jambo hilo alipata kulizungumza bungeni ingawa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha alimpuuza.

“Nilizungumza katika mkutano uliopita wa Bunge kuhusu mipaka ya Ukerewe kuwa wazi sana, nililalamika kwamba, wanajeshi wa Kenya na Uganda wanakuja hadi katika kisiwa hicho kufanya mazoezi yake na kuondoka, lakini nashangaa waziri akanipuuza,” alilalamika Machemli.

Alipotafutwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu kwa ajili ya kuzungumzia juu ya hofu hiyo, alisema anaomba apewe muda kwa sababu yeye ni mgeni mkoani humo na huu mwezi wa pili akiwa katika kituo chake kipya cha kazi, hivyo yapo mengi ambayo hayafahamu.

Hata hivyo, Mangu aliliahidi gazeti hili kufuatilia juu ya suala hilo na kulitolea ufafanuzi baadaye.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mary Tesha alikana kufahamu chochote na badala yake akahoji sababu za mwandishi kumtafuta wakati tayari suala hilo lilisharipotiwa katika gazeti hili hivi karibuni.

Kumekuwa na tetesi za kuwepo kwa vikundi vinavyojihusisha na utoaji mafunzo ya kigaidi hapa nchini, vikiwa vimejificha katika mwamvuli huku lengo halisi likiwa kuhatarisha amani ya kitaifa.

Tayari Rais Jakaya Kikwete amekwishaagiza kusakwa kwa makundi yenye mwelekeo huo yanayohisiwa kuhusika na machufuko na mauaji hapa nchini, wakati akitoa salamu za pole baada ya tukio la kuuawa kinyama kwa Padre wa Kanisa Katoliki Evaritus Mushi huko visiwani Zanzibar.

source Gazeti la Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!