23 August 2014

 

IMEELEZWA kuwa wanawake wanaopata ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kwa kiasi kikubwa inatokana na kufanya mapenzi na wanaume ambao hawajatahiriwa.

Hayo yalielezwa juzi na Mwezeshaji wa mafunzo ya Tohara ya Wanaume kitaifa kutoka katika Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, Nicholous Mbassa wakati wa semina ya siku mbili kwa wanahabari wa mkoani Shinyanga kuhusu masuala ya tohara yaliyofanyika katika wilaya ya Kahama.

Mbassa alisema kwa mwanamume ambaye hajafanyiwa tohara ni rahisi kumuambukiza mwanamke saratani ya shingo ya kizazi wakati wa tendo la ndoa kutokana na uchafu anaokuwa nao.

Alisema ni bora kwa sasa wanaume wakafanyiwa tohara hasa watu wazima, kwani kwa kufanya hivyo kupunguza maambukizo ya ugonjwa hatari wa Ukimwi kwa kiwango cha asilimia 60 pamoja na saratani.

Alisema katika maeneo mengi ambayo watu wametahiriwa, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, yanakuwa na maambukizo machache ya magonjwa kama Ukimwi.

Kwa pande wake Meneja Mradi wa IntraHealth unaosimamia mradi huo ambao unafanya kazi katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara, Innocent Mbulihi, tayari wanaume 295,231 kati
ya 629,000 waliolengwa wametahiriwa.

Alisema pamoja na kuwafikia watu hao, bado wanakabiliwa na changamoto ya kutowapata kwa urahisi wanaume husika, wengine wakikacha kujitokeza kutokana na imani potofu katika jamii wanazoishi.

Meneja huyo aliwashauri wanawake walio katika ndoa huku wakiishi na wanaume ambao hawajafanyiwa tohara kuhakikisha wanawahamasisha waume zao kwenda katika vituo vya kufanyia tohara.

Kuzuia saratani ya shingo ya kizazi

Uchunguzi wa mara kwa mara (screening), mume/mke kutokuwa na wapenzi wengi na kutoanza kujamiiana katika umri mdogo.
Pia kutozaa sana na kutovuta sigara. Muhimu ni kuchukua tahadhari mara uonapo dalili za saratani.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!