24 March 2015

MIIKO NA DESTURI ZETU

Watu wengi kwa kutokujuwa maana na dhamira ya kuweka Miko (Taboo) na makatazo katika mila na tamaduni zetu, wamekuwa wakiona kuwa miko na baadhi ya makatazo kuwa imepitwa na wakati au haikupaswa kuwepo.

Hii inaweza kuwa ni kweli kutokana na maendeleo tuliokuwa nayo hivi sasa, lakini mila na makatazo hayo yalikuwa ni kwa faida kwa walengwa kwa wakati hule na miiko ilisaidia sana katika kudumisha usafi, usalama na kuheshimiana katika jamii.

Kabla ya hatujakosoa mila na tamaduni kutoka kabila lolote inakupasa tutambue kwanini waliweka hiyo miiko, kwenye jamii husika.

Basi kwa kupitia makala hii, tunaweza kuchambua baadhi ya Mila na tamaduni mbalimbali ambazo tunaziona kuwa ni aidha hazikutakiwa kuwepo katika jamii au zilikuwa na lengo aidha kunyanyasa au kumnyanyasa Mwanamke au hata kumshushia hadhi yake. Au tu hazikupaswa kuwepo kutokana na sababu moja au nyingine ambazo msomaji unaweza kuelezea kwa ufupi kwanini unaona kuwa Utamaduni ule, au Mwiko/Miiko ile hakupaswa kufuatwa na jamii husika.

Kwa kuanzia nitachambua baadhi ya makatazo (Miiko) michache ambayo jamii nyingi zimekuwa zikisisitiza kuiheshimu na kuifuata.

Badhi ya miiko ambayo wengi wetu tumekutana nayo kwenye jamii mbalimbali au makabila mbalimbali ni kama hii ifuatayo:

1.    Usipige mruzi usiku, utamwita shetani
2.    Ukisimulia hadithi mchana, utaota mkia
3.    Usikalie Kinu Mwanamke Hutajaaliwa Kuzaa
4.    Ukiona zeru zeru Usimzarau au temea mate kifuani
5.    Usitoe au kuomba chumvi kwa jirani usiku.
6.    Usishone nguo wakati umeivaa, utakua maskini wa kutupwa
7.    Usishone chupi iliyochanika
8.    Mwanamke Mja Mzito haifai kula Mayai (Baadhi ya vyakula), atazaa mtoto Kipara
9.    Usimpige mwenzio kwa nguo
10.    Usimpige mwenzako kwa fagio
11.    Usimruke mwenzako miguu
12.    Kufagia Chumba Usiku kunafukuza bahati (Kama iktokea unafagia usiku basi usitupe taka nje, subiri mpaka asubuhi ndio uzitupe)
13.    Usitupe Nguo Yako ya Ndani Kitambaa Chochote Chenye Hedhi Mbaya Wako Akitupia Jicho Hutozaa
14.    Mwanaume asilie kwenye sufuria la sivyo atakosa mke.
15.    Bundi akitua juu ya nyumba yenye mgonjwa na akali, basi kutakuwa na msiba (Mgonjwa atafariki).

Unapaswa kuelewa kuwa Miiko na makatazo mengi, yalikuwa au yaliwekwa kwa namna ya kumtisha mfanyaji au mkusudiwa ili ajenge woga na kuacha kufanya jambo fulani.
Mfano: Ukitaka kuwatisha wanaume wasinywe/kula kinywaji/chakula fulani basi waambie kuwa kula/kunywa kutawapunguzia nguvu za kiume. Ni rahisi sana kuacha kuliko wangeambiwa kutawapelekea kupata saratani (cancer) japo ndio ukweli.

Mwiko/Katazo:
Usipige mruzi usiku, utamwita shetani.

Maana Na Sababu Yake:
Hii ni kati ya imani ambayo imeanza kipindi kile ambacho machifu ambao walikuwan wakishirikiana na walowezi (Wazungu) kukamata watumwa, upigaji wa miruzi ilikuwa ni njia mojawapo ya kuwahatarisha au kuwataarifu watu kuwa kuna hatari kwa hali hiyo wajihadhari.

Sababu nyingine ni kuwa kipindi cha usiku kuna baadhi ya wadudu hatari kama vile nyoka, ambao wanafutiwa na sauti za miruzi. Kwa wale wanaotoka mikoa ya Tabora, Shinyanga na Mwanza nadhani wana maelezo ya kutosha kuhusiana na upigaji wa miruzi usiku.
---
Mwiko/Katazo:
Ukisimulia hadithi mchana, utaota mkia.

Maana Na Sababu Yake:
Usimuliaji wa hadithi kwa enzi za zamani ni sawa na uangaliaji wa TV au sinema kwa hivi sasa, watu walikuwa wakijishughulisha na utafutaji wa maisha aidha kilimo, biashara, uvuvi au uwindaji na kazi zote hizo zikifanyika kuanzia asubuhi mpaka mida ya jioni.

Sasa usimuliaji wa Hadith kipindi cha mchana, ilionekana ni dalili ya uvivu, na ili watu waogope kusimuliana hadithi kipindi cha mchana ndio ikawekwa kitisho kidogo kuwa ukisimulia au mkisimuliana hadithi mchana unaweza kuota mkia.
---
Mwiko/Katazo:
Usikalie Kinu (Mwanamke) Hutajaaliwa Kuzaa.

Maana Na Sababu Yake:
Kila mtu anaelewa kazi ya kinu, ni kutwanga/kukoboa nafaka, iki ni kifaa muhimu sana na kinatakiwa kupewa heshima yake ili kibakie kwenye hali ya usafi, na ndio maana miko mingi ipo kwenye dhana ya kutishana ili watu waifuate. Ebu mwenyewe fikiria umkute mtu kakalia kitu upande ule wa kutwangia, kisha akipumulie, na kesho atwangie humo humo, uoni kuwa kutaleta hali ya sintofahamu?

---
Mwiko/Katazo:
Ukiona zeru zeru Usimteme mate au ukitema temea mate kifuani.

Maana Na Sababu Yake:
Hapa tuaelekezwa kuonyesha kuheshimiana, kama wewe unamuona zeruzeru ni mchafu au anakuchefua kwa harufu yake au mwonekano wake basi temea mate kwenye nguo yako kama unaweza.
---
Mwiko/Katazo
Usitoe au kuomba chumvi kwa jirani usiku.

Maana Na Sababu Yake:
Chumvi ni bidhaa ambayo rahisi kupatikana, Kipindi hicho kwa mwanamke kupika chakula bila chumvi ilihesabika kama dharau na kutojari kile anacho kifanya. kwa hali hiyo kuishiwa na chumvi kulihesabika kama kutokuwa makini na jiko lako. Ndio maana wanawake kwa kuona hivyo wakatengeneza baadhi ya misamiati ya kuombea chumvi ili waume zao wasitambaue kuwa wameishiwa chumvi Mf: chumvi iliitwa kwa jina la Mkuu wa Jiko, au kwa jina la asili Munyu.
---
Mwiko/Katazo
Usishone nguo wakati umeivaa, utakua maskini wa kutupwa.

Maana Na Sababu Yake:
Kushona nguo wakati umeivaa kulihesabiwa kama ni kujichulia kifo chako. hii ilionekana kama unajishonea sanda mwenyewe. Hii ilikuwa kuwatisha haswa watoto wadogo kwani kushona nguo uku ukiwa umeivaa ni hatari kwao kwani kunaweza kusababisha kujichoma kwa sindano.
---
Mwiko/Katazo
Usishone chupi iliyochanika.

Maana Na Sababu Yake:
Kushona chupi iliyo chanika kulihesabiwa kama ufukara, kwani chupi ni kati ya nguo ambayo ni bei rahisi, sasa ikitokea kwa mwanamke au mwanaume kushona chupi iliyo chanika kulichukuliwa kuwa ni dalili ya Ubahiri.
---
Mwiko/Katazo
Mwanamke Mja Mzito hakutakiwa kula Mayai (Baadhi ya vyakula), atazaa mtoto Kipara.

Maana Na Sababu Yake:
Enzi hizo kulikuwa hakuna hospitali kama hizi za leo, kwa mama mjauzito kula aina ya vyakula vitakavyoweza kumkuza mtoto kiasi cha mama mjamzito kujifungua kwa upasuwaji, vilikatazwa kwa sababu kulikuwa hakuna utaalam wa upasuaji. Kumuachia mama mjamzito kula vyakula hivyo ni kuhatarisha maisha yake nay a mtoto wakati wa kujifungua.
---
Mwiko/Katazo
Usimpige mwenzi kwa nguo.

Maana Na Sababu Yake:
Kumpiga mwenzio kwa nguo kuna weza kusababisha nguo yako kuchanika, ukizingatia kuwa nguo ilikuwa ni bidhaa ghali kidogo. Watu wengi ilikuwa kununua nguo mpya msimu hadi msimu.
---
Mwiko/Katazo
Usimpige mwenzak kwa fagio.

Maana Na Sababu Yake:
Fagio ni kifaa ambacho ni cha kufagilia uchafu, kumpiga mwenzio kwa fagio kunaweza kumletea madhara, kwani utakapo mpiga mwenzio na ukamdhuru aidha kwa kumjeruhi kunaweza kupelekea kupata bakteria au vijidudu vywa maradhi kama vile Pepopunda au Tetenasi.
---
Mwiko/Katazo
Usimruke mwenzak miguu.

Maana Na Sababu Yake:
Watoto walikuwa wakiambiwa si heshima kumruka mtu mzima, ki ukweli si adabu njema na hata kurukana watoto kwa watoto kulihesabika kama yule aliye rukwa kuwa mfupi yaani kutamsababishia kuwa Andunje. Lakini sababu haswa kubwa ilikuwa Kumruka mwenzio miguu ni hatari kwani wakati wewe unataka kumruka mwenzio na yeye wakati huo huo akakunja miguu kunaweza kusababisha mrukaji kudondoka na kuumia vibaya.
---
Mwiko/Katazo
Usifagia Chumba Usiku kunafukuza bahati (Kama ikitokea unafagia usiku basi usitupe taka nje, subiri mpaka asubuhi ndi uzitupe).

Maana Na Sababu Yake:
Kipindi hicho cha zamani ilikuwa kufagia usiku si kwamba kulikatwazwa ila ukifagia usiku haswa chumbani usitupe taka nje, kwa sababu nyumba zilikuwa zinatumia vibatari na mwanga wa kibatari haukuwa kama huu wa taa za umeme, kwa hali hiyo ilikuwa rahisi kwa mtu kufagia kito au kipuri au kitu chochote cha thamani na kukitupa nje bila kujuwa. kwa hivyo basi unapofagia ndani au chumbani usiku takataka unazikusanya pembeni ya chumba na asubuhi yake inakubidi kuzichambua kuangalia kama kuna kitu chochote cha thamani kabla ya kutupa takataka nje.
---
Mwiko/Katazo
Usitupe Nguo Yako ya Ndani Kitambaa Chochote Chenye Hedhi Mbaya Wako Akitupia Jicho Hutozaa.

Maana Na Sababu Yake:
Hapa ni swala zima la afya na usafi wa mazingira kwa sababu mwanamke anatakiwa kuwa msafi, wao na mazingira yao. Hivi kila mwanamke kijijini au mjini au uko mitaani akitupa hizo rocket za kuendea mwezini, sijui hali ya usafi na afya ingekuwaje kama si kuibuka kwa maradhi kwenye jamii.
---
Mwiko/Katazo
Mwanaume kula kwenye sufuria kutamkosesha Mke.

Maana Na Sababu Yake:
Mwanaume kulia kwenye sufuria ni dalili ya ulafi, kinachokufanya mpaka ule kwenye sufuria ni nini? Ndio wakatishwa kwa kuambiwa hayo waliyo ambiwa.

IMANI

Bundi akitua juu ya nyumba yenye mgonjwa na akalia, basi kutakuwa na msiba (Mgonjwa atafariki).

Ufafanuziu Wake:
Wanyama ni viumbe ambao MwenyeziMungu amewajaalia kuwa na hisia kubwa kushinda binadamu.  Wanyama kama Mbwa, Paka, Fisi na ndege kama vile Bundi, au Tai ni wanyama ambao wanauwezo wa kunusa harufu ya mtu au kiumbe ambacho kinakaribia kufa, kwao inawajia kama harufu ya mzoga.

Binadamua au wanyama wanapokasirika au wakiwa na furaha au kukaribia kufa au wakitaka kufanya mapenzi kuna harufu wanatoa ambayo kitaalamu inaitwa Pheromones. (Neno ili pheromone limetokana na maneno mawili ya Kigiriki ‘pherein & hormone ‘pherein’ ikiwa na maana kusafirisha na hormone Kichocheo au kiamsho. Hali hii ni mabadiriko ya kikemikali ambayo utolewa na viumbe hususani wanyama na wadudu.

Vile vile wanyama wanauwezo wa kuhisi majanga ya kiasiri kama vile Vimbunga, mafuriko na matetemeko ya ardhi, majanga ambayo binadamu si rahisi kuyahisi au kuyajuwa mpaka kwa kutumia vyombo vya uchunguzi.

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!