3 January 2015

Shaaban Robert ni mshairi, fasihi  na mwandishi mahiri ambaye anamchango mkubwa katika kuendeleza tamaduni na lugha adhimu ya kiswahili, Shaaban Reobert ni fahari ya Tanzania.

MAISHA YAKE:

Shaaban Robert alizaliwa Januari mosi, 1909 Kijiji cha Vibambani, jirani na Machui, kilomita 10 kusini mwa mji wa Tanga, alipata elimu yake katika Shule ya Msimbazi, jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1922 na 1926, alifaulu na kupata cheti.

Alikuwa mshairi na mwandishi wa riwaya. Mchango wake katika lugha ya Kiswahili ni mkubwa, kwani kazi zake zinaheshimika katika fasihi ya Kiswahili na zinatumika mashuleni. Alifariki dunia Juni 22, 1962.

Aliajiriwa na serikali ya kikoloni akawa karani katika Idara ya Forodha huko Pangani mwaka 1926 – 1944. Bila shaka kukaa kwake miaka mingi hivi katika mji wa kihistoria uliokuwa mahali pa utamaduni wa Kiswahili tena mahali patulivu, kumesaidia maendeleo yake Shaaban kama mwandishi wa Kiswahili.
Tangu mwaka 1944 alihamia ofisi nyingine ya Hifadhi ya Wanyama, baadaye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Mbali na maandiko yake, alikuwa na athari kubwa katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili akiwa mjumbe wa kamati za East Africa Swahili Committee, East Africa Literature Bureau na Tanganyika Languages Board.

Kwa ujumla Shaaban Robert aliandika vitabu ishirini na viwili. Baadhi ya vitabu hivi ni Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu wa Siti Binti Saad, Baada ya Miaka Hamsini, na Maisha Yangu. Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha za Kichina, Kiingereza na Kirusi. Alifariki dunia Juni 22, 1962 na kuzikwa Machui. Aliacha wake watatu na watoto kumi.

Kazi alizofanya alipokuwa karani wa serikali:
Akiwa serikalini alifanya kazi forodhani Pangani na mahali pengine tangu mwaka 1926 hadi 1944; Idara ya Wanyama tangu mwaka 1944 hadi 1946; na Ofisi ya Mkuu wa Jimbo la Tanga tangu mwaka 1946 hadi 1952.

Sehemu zingine ni Ofisi ya Kupima Nchi Tanga, tangu mwaka 1952 hadi 1960.

Alipandishwa cheo kuwa Grade III Higher Division mwaka 1929, na mwaka 1944 alipandishwa tena kuwa Grade II Local Service. Alikuwa mwanachama wa East African Swahili Committee, East African Literature Bureau, Tanganyika Languages, Tanga Township Authority.

Baadhi ya mashairi ya Shaaban Robert:

Kazi bora Afrika, yenye cheo na heshima.
Yapaswa kukumbuka, kuni ukulima.

Vibaya kuzohalika,kushika jembe kulima.
watu wengi wa asili, walikuwa wakulima.

Ubora wa jambo hili, yapaswa kuutazama.
Isipotee asili, makabila yakazama.

Ukulima ni halali, siyo kazi ya lawama.

Shaaban Robert pia alikuwa ni mtetezi wa heshima na haki za wanawake:

Si wajibu kusema, mke hana fadhili.
Wapo waume si wema, tia katika akili.

Na mabaya yanauma, hapana wa kuhimili.
Ukivunja heshima, mke naye hunakili.

ningojeni kina mama, mimi nitawatetea.
Tawatetea lawama, la ovyo lisilo njia

Litaondoka lazima,kwa upesi kukimbia
Mwisho mtajaliwa, nanyi mpewe heshima.

Shaaban Robert pia alikuwa ni mwalimu wa Tabia na maadili mema:

Ambapo anatuambia kuwa thamani ya mtu ni maadili mema si utajiri, nguvu wala ufahari;

Wapo watu maskini, hawana cha kutumia
Lakini wana thamani,kwa ubora wa tabia
Watu hao duniani, ni chumvi ya kutumia
Utatukuka jina, kwa uzuri wa tabia.

Wapo wenye milki, watakavyo hutumia
Lakini si marafiki, kwa ubaya wa tabia
Hao hawachukuliki,hatari kukaribia
Utatukuka jina, kwa uzuri wa tabia.

KIFO CHAKE

Marehemu Shaaban Robert alifariki Tanga Juni 22, 1962, alizikwa Machui, Tanga. Alituzwa zawadi ya waandishi inayojulikana kama ‘Margaret Wrong Memorial Prize’na nishani ya M.B.E.

Mungu ilaze roho ya Shaaban Robert mahala pema peponi.

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!