22 October 2014

Serikali ya Tanzania, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani, inatathmini uwezo wake wa kupima Ebola, gazeti la Daily News la Tanzania liliripoti Jumanne

Tanzania haina Ebola, ingawa mkaazi mmoja wa Sengerema aliyeugua akiwa na dalili kama za Ebola alikufa hospitalini wiki iliyopita, alisema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Evarist Ndikilo.

"Hospitali ya Wilaya ya Sengerema ilimpokea marehemu Salome Richard, ambaye alitokea katika Kituo cha Afya cha Mwandike, na vipimo vilipelekwa mara moja Nairobi kwa upimaji wa kitaalamu zaidi," Ndikilo alisema.

Hivi karibuni Tanzania itaanza kupima katika maabara ya kitaalamu huko Mbeya ili kujua kama Richard aliambukizwa Ebola, alisema Ofisa Mkuu wa Maabara ya Mkoa Justina Malima.

Upimaji huo utatumika kutathmini kama upimaji wa Ebola unaweza kufanyika nchini Tanzania badala ya kupelekwa huko Nairobi.

Ndliko aliiomba Idara ya Bohari ya Madawa kusambaza dawa zinazotakiwa na vifaa vya kujikinga kwa hospitali za mkoa.

Alisema kampeni za uelimishaji pia zijumuishe vipindi katika redio za jamii na kupitia mitandao ya kijamii.

Zaidi ya wafanyakazi wa afya 820 katika mkoa wa Mwanza wamepata mafunzo katika utaratibu wa matibabu ya Ebola na vipeperushi zaidi ya 13,700 vimesambazwa kama sehemu ya hatua za tahadhari za mkoa.

Wakati huo huo Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete alitangaza siku ya Jumanne kwamba serikali itatumia shilingi milioni 931 (Dola 560,000) kusaidia mapambano dhidi ya Ebola, gazeti la The Guardian la Tanzania liliripoti.

Rais  Kikwete alitoa tamko hilo baada ya kutembelea kituo cha matibabu kilichotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola katika Hospitali ya Mkoa ya Temeke huko Dar es Salaam na kukagua vifaa vya kupima joto vilivyofungwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

"Nimeridhishwa na matayarisho yote ya kituo kilichotengwa kwa ajili ya matibabu na ufungaji wa vifaa vya kupimia joto," alisema. "Nitamuelekeza waziri wa fedha kutoa fedha haraka iwezekanavyo."

Madaktari wawili wa Tanzania pia walijitolea kusaidia huko Liberia, na watapelekwa hivi karibuni, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Seif Rashid alisema.

Wakati huohuo, Kenya imewaondoa wasafiri 12 ambao waliwasili nchini humo kutoka Sierra Leone, Guinea na Liberia tangu tarehe 19 Agosti, gazeti la Daily Nation la Kenya liliripoti.

Wasafiri wote wanaoingia sasa wanapimwa kwa ajili ya dalili za Ebola, Mkurugenzi wa Afya ya Umma wa Kenya Kepha Ombacho alisema.

"Kwa pamoja na viongozi wa afya na uhamiaji bandarini, tumeimarisha upimaji na uchunguzi katika bandari vituo vya kuingilia ili kupunguza hatari ya Ebola," alisema.

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!