12 November 2014

MWANDISHI wa gazeti la Jamboleo kutoka mkoani Iringa Bw Francis Godwin ameteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama cha Wamiliki Mitandao ya Kijamii (Blogs) nchini Tanzania.

Godwin ambae ni mmiliki wa blog ya "MatukioDaima" na "FrancisGodwin" ameteuliwa katika nafasi hiyo kama mwakilishi wa wamiliki wote wa blogs za mikoani, huku Joachim Mushi akiteuliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Uteuzi huo umefanyika leo katika ukumbi wa Mlimani City baada ya kumalizaka kwa warsha ya siku moja iliyoandaliwa na mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA).
Wengine walioteuliwa ni pamoja na Katibu wa chama hicho Khadija Kalili, ambapo wajumbe ni Mdimu Henry, William Malecela, Othman Maulid na Shamim Mwasha.

Akizungumza mara baada ya uteuzi huo mwenyekiti wa chama hicho Bw Mushi alisema kuwa lengo ni kuhakikisha katiba ya chama hicho inakamilika mapema zaidi ili chama hicho kiweze kusajiliwa rasmi.

Mkurugenzi mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema kuwa mamlaka yake itasaidia kufanikisha mchakato mzima wa wamiliki wote wa blog nchini kuwa na chama chao na kuwa lengo ni kuwawezesha kufanya maamuzi yao kwa umoja na kuweza kusimamiana wenyewe.

Profesa Nkoma alisema kuwa iwapo wamiliki wa blogs nchini wataanzisha chama chao upo uwezekano mkubwa wa TCRA kuwasaidia mchakato huo na pia kuendelea kuungana na chama hicho kwa kuendelea kutoa elimu zaidi.

Mbali ya kuwataka kuanzisha chama hicho,  bado aliwataka wamiliki wa blog nchini kuendelea kuifanya kazi hiyo kwa kuheshimu misingi ya maadili badala ya kutumia vyombo hivyo kuvuruga maadili.

Akielezea kuhusu uwajibikaji wa blogs nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, alitaka kuhakikisha wanatoa nafasi sawa kwa vyama na wagombea wote bila upendeleo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa idara ya habari (Maelezo) Assah Mwambene aliwataka wanahabari nchini na walimiki wa blogs kuendelea kuutumia vyema uhuru wa vyombo vya habari na kuangalia mambo ya msingi kwa jamii badala ya kugeuza mitandao hiyo kuvuruga amani ya nchi.

Safu ya Uongozi:

  • Mwenyekiti: Joachim Mushi
  • Makamu Mwenyekiti: Francis Godwin
  • Katibu: Khadija Kalili
  • Wajumbe: Shamim Mwasha, Mdimu Henry, William Malecela, Othman Maulid
Reactions:

0 comments:

Post a Comment

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!