25 January 2014

HUU ni ukatili uliopitiliza! Wakati  wanaharakati mbalimbali nchini wakiwemo wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) wakipinga vikali vitendo vya ukatili, baba  wa kufikia, Musa Mdetela, mkazi wa mjini hapa anasakwa na polisi kwa kosa la kuwachoma moto miguuni wanaye wa kambo.

Mdetela anadaiwa kuwafanyia unyama huo watoto hao, Baraka anayesoma darasa la kwanza na Mudi wa darasa la sita  baada ya kuwatuhumu kuwa, waliiba shilingi 10,000.
Wakizungumza na mwandishi wetu wakiwa katika sura ya huzuni, watoto hao walisema baba huyo aliwatendea unyama huo Januari  3, mwaka huu ambapo walijitetea kuwa walichukua ‘teni’ hiyo kwa ajili ya kununulia msosi baada ya mama yao kushindwa kuwaandalia chakula.

Hata hivyo, Mudi alisema siku ya  tukio mdogo wake (Baraka) aliingia chumbani kwa baba yao na kuchukua kiasi hicho cha fedha kisha wakashirikiana katika matumizi ambapo walinunua bagia na vitumbuia ili wajipoze kwa njaa.

Wakizungumzia kuhusu baba yao mzazi (jina tunalo), walisema aliwaacha mkoani hapa kwa muda mrefu na sasa anaishi jijini Dar es Salaam hivyo wao wamebaki na baba mdogo huyo ambaye mara kwa mara amekuwa  akiwaadhibu vikali na kuwanyima chakula.

Kwa masikitiko makubwa, walisema baada ya baba yao kurudi kutoka kwenye shughuli zake na kubaini katika akiba yake  teni haipo ndipo alipowakamata na kuwafunga kamba na kuanza kuwatesa kwa kichapo ili waseme mtu aliyekwapua pesa hiyo.

“Alitufunga kamba miguuni na mikononi na kuanza kututesa kwa kutupiga. Alipoona hatusemi, akachukua manailoni na kutufunga miguuni kisha akachukua kiberiti na mafuta ya taa na kuwasha moto miguuni kwetu.

“Tulilia sana, akaendelea kutupiga na moto ukiwaka. Wakati huo mama alikuwa amekaa mlangoni akishangilia na kusema wapige sana mimi nimewachoka hao watoto, heri wafe tu,” walisema watoto hao.

Imedaiwa kuwa baada ya kutekeleza unyama huo, baba huyo aliwafungia ndani watoto hao na kuwaambia wasitoke nje ndipo majirani walioshuhudia tukio hilo walipotoa taarifa polisi katika kitengo cha dawati la jinsia wakalivalia njuga swala hilo.
Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Iringa, Atupele Mwambunda alizungumza na mwandishi wetu na kusema wamefanikiwa kumkamata mama wa watoto hao, Watende  Sanga huku mumewe, Mdetele aliyekimbia akitafutwa kwa udi na uvumba ili kufikishwa kwenye mikono ya sheria.
Akiwa katika ofisi za dawati la jinsia, mama  wa watoto hao alidai wakati baba yao mdogo akiwapa mbata watoto hao yeye hakujua kinachoendelea japokuwa alipata taarifa ya kupotea kwa pesa.

Aliendelea kusema kuwa, baada ya tukio hilo aliwanunulia dawa watoto hao ili kuwatibu kinyemela pamoja na kuwaombea ruhusa shuleni.
Mwanamke huyo aliomba kusamehewa kwa vile hakujua kama kushangilia wakati baba yao akiwapa adhabu watoto hao ni kosa. Anaendelea kushikiliwa na polisi mkoani hapa.

 Chanzo GPL

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!