8 July 2013

Mafuta ya Ubuyu ambayo yamejitwalia umaarufu siku za karibuni kiasi cha kufanya yawe ya bei mbaya sana yameelezwa kuwa si salama kwa afya..

TFDA wamepiga marufuku kwa kuwa yana Tindikali ya mafuta, na anayekunywa kwa wingi ana hatari ya kupata Kansa za aina mbali mbali.

TDFA inaonya jamii kuwa mafuta hayo si mazuri na si salama na inashauri watanzania kuacha kutumia.

HABARI KAMILI HII HAPA KUTOKA HABARI LEO

Imechapishwa Jumatatu, 08 Julai 2013 | Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko

BAADA ya kuonya wananchi wanaotumia dawa za tiba mbadala ambazo hazijathibitishwa, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), sasa inawataka wananchi kuacha kutumia mafuta ya ubuyu kwa kunywa kama dawa.

Akizungumza na gazeti hili juzi katika Maonesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza, alisema Mamlaka hiyo ilipima na kubaini mafuta hayo yana tindikali ya mafuta.

Alifafanua katika maonesho hayo maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, kwamba mafuta hayo hayafai kuliwa na binadamu na anayekunywa kwa wingi, yuko hatarini kupata saratani za aina tofauti tofauti.

“Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la wajasiriamali wanaouza mafuta ya ubuyu kama dawa, kwa kuwaelekeza wananchi kunywa. Napenda kuwataarifu kuwa mafuta hayo ni hatari kwani yana tindikali ya mafuta,” alisema.

Gazeti hili lilipata sampuli ya vielelezo vya matumizi yake na manufaa yake mwilini, kama inayotangazwa na wajasiriamali katika maeneo mbalimbali na hata katika mitandao.

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!