14 October 2012


Na. Mahmoud Zubeiry

WIKI hii mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Danny Davis Rwanda alichangia habari niliyoandika kuhusu mshambuliaji wa Simba kutoka Ghana, Daniel Akuffor.

Habari ilikuwa inamnukuu kocha wa Simba, Profesa Milovan Cirkovick akisema kwamba Mghana huyo kwa sasa hapangwi katika kikosi cha kwanza kwa sababu wanaopangwa wanamzidi uwezo.
Mrwanda, akiwa miongoni mwa watu wa awali kabisa kuchangia, akaandika; “Tatizo 20 percent kaka”akimaanisha tatizo ni asilimia 20.

Baadaye niliwasiliana binafsi na Mrwanda kumuomba anifafanulie juu ya alichochangia, lakini akagoma.

Hata hivyo, kwa mtazamo wa wengi ni kwamba, hivi sasa Simba ili ucheze lazima ukate asilimia 20. Ya nini? Sijui!

Hii si mara ya kwanza mimi kusikia malalamiko kama haya kutoka kwa wachezaji, ambao wapo katika wakati mgumu Simba- wakidai kuna viongozi wanapeleka wachezaji wao kwenye timu hiyo hata kama hawana uwezo, ili mradi tu wanakata asilimia 20.

Wakati fulani Yanga ilipokuwa chini ya kocha Mserbia, Profesa Dusan Savo Kondic kulikuwa kuna kashfa kama hii ya asilimia 20, ambayo ilihusu fedha za usajili na mishahara. Yussuf Manji, mfadhili wa Yanga, aliifanyia kazi vizuri kashfa hiyo na alipogundua akachukua hatua, watu walipoteza kazi Jangwani.

Wachezaji walioachwa Simba baada ya msimu uliopita wengi wao wanalalamikia hiyo asilimia 20 na baada ya kuwa malalamiko ya chini chini, hatimaye sasa yanaanza kuwekwa hadharani.
Mrwanda anayelalamikia asilimia 20, ni ambaye alikuwemo kwenye kikosi cha Simba cha msimu huu, akisajiliwa tena kutoka Vietnam alipokuwa anacheza soka ya kulipwa, lakini akaachwa dakika za mwishoni kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.

Nilijiuliza, kweli Mrwanda alikuwa katika kiwango cha kuachwa Simba? Mrwanda yule ambaye Simba ilimsajili ikimgombea dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga?

Mrwanda yule ambaye alitokea benchi kwenye Fainali ya Kombe la Urafiki, Simba ikiwa nyuma kwa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC na kwenda kusababisha penalti iliyoipa Simba bao la kusawazisha na hatimaye kutwaa Kombe hilo kwa mikwaju ya penalti?

Yakawa yanaibuka majibu ya pembeni, eti Mrwanda kiburi sana ameshindwana na kocha, yaani Milovan. Labda!
Lakini sasa Mrwanda anafunguka, baada ya kimya kirefu anasema tatizo ni asilimia 20. Amri Kiemba amepata tabu sana kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha Simba msimu huu na sasa anaisaidia sana timu.

Amri alirudishwa uwanjani, baada ya kuonekana kabisa timu ina tatizo katika nafasi ya kiungo wa ulinzi- hakukuwa na jinsi amerudishwa na anaonyesha umuhimu wake kwa kuibeba sana timu na kuwaacha ‘visokorokwinyo’ vichwa chini kwa fedheha.

Bado najiuliza, mshambuliaji Abdallah Juma ‘Dullah Mabao’ kwa nini hapangwi katika kikosi cha kwanza cha Simba, wakati dogo alionyesha uwezo mkubwa sana kuanzia kwenye michuano ya Kombe la Urafiki hadi Kombe la Kagame.

Huyu kijana amekuwa akipigwa mizengwe tangu wakati anataka kusajiliwa akitokea Ruvu Shooting, lakini Mungu wake alimsimamia. Ila sasa hachezi na haumwi, kwa nini?
Simba ni bora sana na ndio maana ni mabingwa wa Tanzania na klabu yenye rekodi nzuri zaidi katika michuano ya Afrika- lakini inaweza kuwa bora zaidi iwapo baadhi ya mambo yanayokwenda kinyume na maadili yataondolewa katika klabu hiyo.

Yupo mtu mmoja aliwahi kuniambia; “Huyu Paul Ngalema hata awe mzuri vipi, hawezi kucheza Simba, kwa sababu mwenye namba yake mjomba wake ni kiongozi wa Simba na ndiye aliyemsaidia kuingia Simba, baada ya kufukuzwa Yanga,”.

Japokuwa nilimpuuza kwa kuwa naamini viongozi hawawezi kumuingilia kocha, lakini kwa kauli hii ya Mrwanda sasa naanza kupata shaka kuna mambo yaliyo kinyume cha maadili yanaendelea Simba SC.

Naamini ndani ya Simba hakuna mtu mwenye nguvu kuliko Simba yenyewe- hivyo ipo haja kwa uongozi wa klabu hiyo hivi sasa ukayafanyia uchunguzi madai haya, ili kama yana ukweli wowote hatua ichukuliwe, ili kuisafisha klabu.

Hivi kweli leo, Mrwanda na Akuffo waitwe kufanya majaribio timu moja, nani atafuzu jamani au turudie mara mbili mbili uchezaji wa Abdallah Juma na huyo Mghana, nani anastahili kutokea benchi kwenda kuiongezea nguvu timu japo kwa dakika 20 za mwisho?

Katika uongozi, kama kuna jambo la msingi sana, kwanza ni maadili. Kama viongozi wanakuwa siyo waadilifu basi timu haitakuwa na misingi imara hata kidogo. Hivyo basi, ipo haja uongozi wa Simba, kuifanyia kazi kashfa hii ili kama ni kweli ipo, hatua zichukuliwe.

Wakati fulani niliwahi kufanya mahojiano na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe akaelezea mfumo mzima wa utendaji wa Kamati yake- kwamba yenyewe inapokea mapendekezo ya Kamati ya Ufundi na benchi la ufundi juu ya usajili na kutekeleza jukumu la kusajili.

Lakini Hans Poppe akasema kuna wachezaji ambao wamekuwa wakiingia kinyume cha utaratibu uliowekwa na bila shaka tatizo linaweza kuwa linaanzia hapo.

Uadilifu ni tatizo kubwa sana katika soka yetu, watu wanaingia madarakani na miili kama ya wanariadha wa mbio ndefu, lakini baada ya miezi sita wanafutuka kama warusha matufe. Mungu ‘amrehemu’ hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati wake alisimamia uadilifu kikamilifu na alichukua hatua kali dhidi ya viongozi waliokosa uadilifu- si tunakumbuka enzi zile za staafisha kwa manufaa ya umma?

Leo ni miaka 13 tangu tumpoteze baba wa taifa letu, tunaishuhudia Tanzania tofauti, iliyokithiri utovu wa maadili na uzalendo, kwenye soka ndiyo balaa! Wito kwa Simba SC, wamuenzi mwalimu Nyerere kwa kupambana na hawa 20 Percent, ili kusafisha hadhi ya klabu yao!

Kwa habari zaidi za michezo ingia http://www.bongostaz.blogspot.com

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!