23 April 2012

Ndugu zangu,
Katika dunia hii mwanadamu huwezi kumchagua jirani yako. Jirani yako ni jirani yako. Msiba wa jirani ni msiba wako pia, unakuhusu.
Maana, kuna wanaohoji JK kuacha mambo ya nyumbani na kwenda kushiriki maziko ya Bingu wa Mutharika. Silioni kosa katika hilo. Na hata kama JK angeamua kutokwenda mazikoni Blantyre, bado, asingekwepa lawama. Maana, kuna ambao wangemlaumu JK kwa kutozingatia mila na desturi zetu Waafrika; kushiriki kwenye kumzika jirani yako. 
Tukumbuke, kuwa Wamalawi si tu ni jirani zetu, ni ndugu zetu pia. Kuna Wanyasa wengi wa Malawi katika nchi hii waliochanganyika na makabila yetu. Na tunaambiwa, kuwa siku ya mkesha wa Uhuru wa Malawi, Watanzania wengi kando ya Ziwa Nyasa nao walikesha wakishangilia. Uhuru wa Mnyasa ni Uhuru wetu. Msiba wa Mnyasa, ni msiba wetu.
Mengineyo...
Nchi yetu inapita sasa kwenye kipindi kigumu sana. Tusishushe chini kiwango cha mjadala. Kubaki kumjadili JK na safari kwenda kutuwakilisha mazikoni ni kushusha kwa makusudi kiwango cha mjadala. Kwa makusudi tutakuwa tumeacha kujadili hoja za msingi ikiwamo hii ya kashfa za ufisadi wa kutupwa uliodhihiri bungeni na unaotutaka tuweke shinikizo kwa wahusika kuachia ngazi na hata kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Maana, anayeliibia taifa ni mhalifu tena zaidi ya mwizi wa kuku. Huyu ni jambazi. Kumwacha aendelee kukalia ofisi ya umma ni sawa na kumsusia mlevi bia, au kumpa fisi kazi ya kulinda bucha.
Tuliko sasa ni kubaya. Tunakokwenda kutakuwa ni kubaya sana kama hatutachukua hatua sasa. Nimeona asubuhi ya leo kwenye runinga ( Channel Ten) utetezi wa ajabu kutoka kwa Waziri wa Uchukuzi Bw. Omar Nundu.  
Nundu anadai hawezi kujiuzuru kwa kutoa hoja ambazo kimsingi zinamtaka aachie ngazi haraka iwezekanavyo ili abaki na heshima kwa jamii kama bado anayo.
Anatwambia Watanzania kuwa amekuwa 'akizungukwa' na Naibu wake Athuman Mfutakamba. Ndio, Waziri Nundu anapojitetea kwa Watanzania kwa kusema haelewani na Naibu wake na kuwa kampuni ya Kichina ilimpeleka Naibu wake China, Mauritania na Equatorial Guinea bila kibali chake inatosha kuonyesha kiwango cha juu cha ukosefu wa nidhamu, uwajibikaji na uadilifu katika baraza la mawaziri . Sioni ni kwa namna gani maelezo ya Nundu yanaweza kumlinda mbali ya kuonyesha ulazima wa kuwajibishwa kwake haraka iwezekanavyo.
Ndio huwezi kuonyesha kuwa ulijua kilichokuwa kikifanyika, ukabaki kimya mpaka unatwambia hii leo, halafu utake ridhaa ya umma ikuamini kuendelea kukupa dhamana ya kushika nafasi hiyo hiyo.
Na wahenga walisema; kwenye msako wa nyani ngedere hawezi kusalimika.
Ndio, tutafanya makosa kudhani kuwa ’madudu’ haya yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya CAG yanahusu Wizara tano au sita tu. Hii ni fursa pekee kwa Watanzania kupitia wabunge wao kuendesha ’ msako mkubwa’ wa wote wenye kulitafuna taifa letu tunalolipenda.
Ni wakati pia wa kuhakikisha Katiba Mpya tunayokwenda kuitolea mapendekezo yetu itusaidie kuziba mianya ya wezi wa mali ya umma kuendelea kuliibia taifa bila ya hofu ya kufikishwa mahakamani na hata kutiwa magerezani.
Ndio, hatuwezi kuenenda kama tunavyoenenda sasa; maana, unapoona Wananchi wanalalamika, Wabunge wanalalamika, Mawaziri wanalalamika, na Rais analalamika, basi, hilo ni taifa la ajabu sana. Taifa la Walalamikaji.
Na maradhi ya ' kulalamika' ni ya kimfumo. Ni mfumo mbovu tu ndio unaoweza kuzaa Taifa la Walalamikaji. Turekebishe mfumo wetu kwa kupitia Katiba. Inawezekana.
Maggid Mjengwa,
Iringa.

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!