26 February 2014

                 Salma akiwa kazini

Nimekuwa nikipitia blog na website za watu wote wanaoitwa maarufu walau kila siku katika maisha yangu,lakini zipo baadhi ya blog/website ambazo hunifundisha ninapoingia na kuna ambazo hunifurahisha.

Lakini Salma Msangi website ni moja kati zile zinazonifundisha kitu labda ni kutokana na stori ambazo zinaandikwa humo.

Leo hii katika pita pita yangu mitandaoni nimekutana na mahojiano yake na moja ya blog ya hao watu maarufu,mahojiano yote nimeyapenda hasa jinsi Salma alivyojibu maswali lakini Kwangu mie haya maswali mawili ndio niliyoyapenda zaidi


BC: Inajulikana kwamba wewe ni miongoni mwa watu wenye ushawishi na umaarufu katika jamii na ambao wapo ndani ya ndoa. Ukichanganya kazi yako,nyumba,familia nk unawekaje yote sawa?

 

Salma: Naweza. Ndoa sio kifungo. Ni makubaliano baina ya watu wawili. Ndoa haina formula kwamba lazima uwe hivi au vile. Kikubwa ni kujiheshimu maana suala la kujiheshimu si tu mpaka uwe kwenye ndoa. Kwa ujumla mwanadamu unatakiwa ujiheshimu na uwe mwaminifu kwa maamuzi uliyoamua. Ndoa ni mapenzi ya mkataba baina ya watu wawili waliopendana. Sasa kama unajua hutaweza kuwa muaminifu basi kwanini ukubali mkataba huo?


              Salma na Mumewe

Ndoa kwangu ni vile ninavyoishi na mwenzangu.Tunapendana, tunaelewana, tunaheshimiana, tunaaminiana na tunavumiliana. Kila mmoja anakubali anachokifanya mwenzie bila kwenda kinyume na matakwa yetu wawili. Ndivyo ndoa yangu ilivyo. Mimi ni Salma Msangi kwenye kazi yangu vile utakavyoipokea.

 

Baada ya kazi mimi ni mke, mama wa familia ninayetambua majukumu yangu. Sina watoto kwa sasa wa kuwazaa lakini nina watoto wa kuwalea, wadogo zangu ambao mimi najivika kilemba cha ulezi. Watoto hawa wanahitaji malezi na makuzi mazuri na mimi kwao kama mfano kwao. Sasa kama nitaenda kinyume sitakua mzazi mlezi mwema. Wazazi wangu walinilea vizuri na kuniamini kunipa wadogo zangu kutokana na kuamini kutokana na malezi yao. Sitaki kuwaangusha wazazi wangu.

 

Mimi kama mwanamke niliyeolewa na mfanya kazi, ninayajua na kuyafahamu majukumu yangu. Najua kutofautisha muda wa kazi, muda wa familia, muda wa marafiki, muda wa jamii nk. Na ninapata muda wa kupumzika pia.

 

Kila kitu ni kuamua kutoka rohoni. Mtazamo wa mtu wa nje sio wa kum-judge. Maisha ni namna unavyoishi ili mradi usivunje sheria. Kuwa na mfumo wako na sio kwa sababu ya watu. Jifurahishe. Fanya unachokipenda maana maisha aliyoishi baba yako na mama yako sio yako au ya leo. Au maisha ya rafiki yako na mkewe au mumewe sio yako. Kila mtu ana utaratibu wake. Msiitafsiri ndoa vibaya.

 

BC: Inajulikana kwamba bado unajishughulisha na masuala ya urembo nk. Ni wabunifu gani wa mitindo unaofurahia au kuzipenda kazi zao zaidi? Unaweza kunitajia wa nyumbani Tanzania au nje ya Tanzania.

 

Salma: Samahani lakini kwa Tanazania sioni jipya. Siku zote nasema Tanzania hakuna wabunifu, kuna washona nguo. Imezoeleka mafundi cherehani japo si watengeneza cherehani mie nitawaita washona nguo. Katika suala la kubuni hapa hapo watanisamehe tuna safari ndefu.


Tunahitaji ubunifu zaidi na si kuchukua catalog za nje tunashona kisha models wanapita Runway tunasema ni ubunifu wa Tanzania. Nje ni wengi na wanajieleza kikubwa tuige mifano yao ila tubaki kwenye tamaduni zetu.

Ukitaka mengi kuhusu haya mahojiano ingia www.bongocelebrity.com








0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!