28 December 2013

Miaka hii ya karibuni tukizungumzia wakimbizi, akili zetu zinatupeleka Congo, Burundi, Somalia, Iraq na nchi zingine ambazo zinatajika kwenye vyombo vingi vya habari.


Je unaweza kuamini kuwa nchi za Ulaya nazo ziliwahi kutoa wakimbizi, na wakimbizi hao kuifadhiwa katika nchi za Afrika, tena Afrika Mashariki?

Wengi wetu hatuna habari wala hatufahamu kuwa Tanzania iliwahi kupokea wakimbizi kutoka Poland, wakimbizi ambao walihifadhiwa katika mji wa Arusha uko Tengeru.


Kiukweli ni miaka kadhaa imepita sasa tangia wakimbizi hao walipoifadhiwa, kulikuwa na idadi ya wakimbizi wasiopungua elfu tano (5 000), ambao walipewa hifadhi katika nchi ya Tanzania wakati huo ikiitwa Tanganyika koloni la Mwingereza.

Bara pekee ambalo lilikuwa salama wakati wa vita kuu ya kwanza na ya pili ilikuwa ni Afrika, kwa maana ya Afrika Mashariki.


Serikali ya Muingereza, ilijenga vituo vingi vya wakimbizi visivyo pungua elfu ishirini (20 000) kwenye makoloni yake. Na moja ya makoloni ya Kiafrika yaliyopata bahati ya kupokea wakimbizi wa kutoka ulaya (Poland) ni Tanganyika, Kenya na Uganda.

Ukifika eneo ili utakutana na kibao kimeandikwa "Cemetery of Polish War Refugees 1942-1952". “Makaburi ya Kipolish ya wakimbizi wa vita 1942-1952”
Mahali hapo kuna makaburi yasiopungua 148 mengi yao yakiwa ni ya waumini wa kikatholiki, Orthodoksi na Wayahudi.


Makaburi yote hayo 148 ni ya wakimbizi, ambao wengi waliathirika na magonjwa ya Maralia na mafua na maradhi mengine.

Kabla ya hapo wengi wao walikuwa ni watumwa waliofanyishwa kazi na mateso uko Urusi katika jimbo lenye baridi kali sana la Siberia.

Ilikuwa ni tarehe 1 Septemba mwaka 1939 majeshi ya Nazi (Ujerumani) yalipovamia kwa ghafla nchi ya Poland kipindi cha mwanzo wa vita kuu ya pili ya dunia.

Karibia nusu ya nchi ya Poland ilichukuliwa na Umoja wa Kisovyeti (sasa Urusi) na hali hii ilipelekea watu wengi haswa wanaume na wanawake wenye afya zao kuchukuliwa na kupelekwa kufanyakazi za kitumwa uko Urusi katika jimbo la Siberia, hatua hii ya kuchukuwa watu ilianza tarehe 10 Februali 1940, baada ya makundi ya kisomi na wenye vipato kuanzisha harakati za upinzani.


Mwaka 1942 wakati majeshi ya Ujerumani yanavamia Poland, serikali ya Kipolishi wakishirikiana  na umoja wa Kisovyeti  wakaanza kuwarudisha wahamiaji wa Kipolishi, wapatao elfu arobaini na saba (47 000) waliohamishwa Siberia. Wengi wao walipelekwa kwenda kuishi kwenye makoloni ya Muingereza, na wakimbizi wapatao elfu kumi na nane (18 000) wa Kipolish walihamishiwa kwenye makambi ya wakimbizi yaliyoko Afrika.

Tanganyika peke yake kulikuwa na kambi sita (6), na kambi kubwa kuliko zote ilikuwa Arusha katika kijiji cha Tengeru, kambi ambayo ilikuwa na wakimbizi wapatao elfu tano (5 000).


Matajiri ambao walikuwa ni walowezi wa Kipolish, hawakukaa tu na kusubiri huruma ya serikali ya mkoloni (Muingereza) walijitahidi na kufanya shughuli za kimaendeleo ili kuendesha maisha yao, walilima mashamba, wakafanya biashara ndogo ndogo, wakafungua na shule kadhaa. Wakajengwa kliniki, na hospitali, makanisa na sinagogi moja.

Baada ya vita ya dunia kwisha, wakimbizi wengi walirudi Ulaya, lakini wengi wao hawakuwa na mahali pa kwenda, sababu ndugu na jamaa zao karibia wote aidha walikuwa wamekwisha fariki kutokana na vita au walikuwa uhamishoni. Na wengine walikuwa bado na hofu ya kuchukuliwa tena na kupelekwa kwenye makambi ya mateso uko Urusi na Ujerumani.

Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kuwa takribani wakimbizi elfu moja (1 000) walibakia na kufanya makazi yao Afrika, na wakimbizi wasiopungua mia moja na hamsini (150) walibakia Tengeru.

Baadhi ya Wanakijiji wachache hapo Tengeru wanajuwa kuwa kuna makaburi ya walowezi wa kipolish, lakini ni Watanzania wangapi ambao wanajuwa kuwa Tanzania ilipata bahati ya kuhifadhi wakimbizi wa KIpolish wasiopungua elfu tano ( 5000)?

Wakati dunia nzima iliwatelekeza wakimbizi hawa, lakini wakajikuta wakiletwa kwenye kisiwa cha amani Tanzania na kuishi bila ya wenyeji wengi kujuwa.
 
Makaburi hayo ya Kipolish yanahifadhiwa kwa pesa zitokazo kwenye serikali ya Poland...

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!