16 June 2014


Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, imemhukumu kifungo cha miezi tisa jela, Haven Robert(24) baada ya kupatikana na hatia ya kumwibia mpenzi wake Sh 3.9 milioni.

Pia mahakama hiyo, imemwamuru Haven kumlipa kiasi hicho cha fedha mlalamikaji Frank Malele ambaye ni mpenzi wake mara atakapotoka kifungoni.

Mwanamke huyo ambaye ni mkazi wa Tabata Mawenzi, atatumikia kifungo hicho baada ya kupatikana na hatia ya kumwibia mpenzi wake wakati wakiwa hoteli walikokuwa wamepumzika.

Akitoa hukumu jana, Hakimu Matron Luanda alisema mshtakiwa atatumikia kifungo hicho baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo. Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea, ambapo mshtakiwa alidai kuwa ana familia inayomtegemea.

Hata hivyo, baada ya mshtakiwa kuomba mahakama impunguzie adhabu, karani Shao aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wanawake wenye tabia ya kuwaibia wapenzi wao.

Kutokana na ombi la karani huyo, hakimu Luanda alimhukumu mshtakiwa huyo kifungo hicho ili iwe fundisho kwa wanawake wenye tabia kama hizo.

Awali karani wa mahakama hiyo, Blanka Shao alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo April 6, mwaka huu katika Hotel ya Colombia iliyopo Kariakoo Wilaya ya Ilala.

Shao alidai siku ya tukio saa 9:30 usiku katika hoteli hiyo, mshtakiwa alichukua fedha hizo zilizokuwa zimehifadhiwa katika kabati iliyokuwapo ndani ya chumba cha hoteli hiyo, wakati mpenzi wake akiwa amelala.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!