Kamati hiyo ya umoja wa Mataifa imesema maelfu ya watoto kote duniani wamedhalilishwa kingono kwa miaka mingi ndani ya kanisa katoliki.Katika ripoti inayolishutumu vikali kanisa hilo,kamati hiyo imesema kanisa katoliki limeshindwa kwa kiasi kikubwa mno kutekeleza ahadi yake ya kukomesha visa vya unyanyasaji kingono dhidi ya watoto vinavyofanywa na makasisi na wafanyakazi wa kanisa hilo ndani ya makanisa na shule zinazosimamiwa na kanisa hilo.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa inatiwa wasiwasi mkubwa na hatuwa ya makao makuu ya kanisa katoliki Vatican ya kutokubali ukubwa wa uhalifu uliofanywa na haijachukua hatua muafaka za kukabilana na unyanyasaji wa watoto ili kuwalinda na badala yake imeanzisha sera ambazo zimesababisha kuendelea kwa udhalilishaji huo bila ya kutojali.
Watuhumiwa wanalindwa na kanisa.
Umoja wa Mataifa umeshutumu hatua ya kanisa hilo kuwahamisha makasisi wanaotuhumiwa kutoka parokia moja hadi nyingine ndani ya nchi na hata wakati mwingine kuhamishiwa nchi nyingine katika juhudi za kufunika maovu hayo na kuwakwepesha kukabiliwa na mkono wa sheria.
Makao makuu ya kanisa hilo yametoa taarifa baada ya ripoti hiyo ya umoja wa Mataifa na kusema imesikitishwa na kile ilichokiita hatua za kuingiliwa kwa mafunzo ya kanisa hilo kuhusu uavyaji mimba na matumzi ya mpango wa uzazi.
Mwanakamati wa kamati ya kutetea haki za binadamu ya umoja wa Mataifa Kirsten Sandberg
Vatican imesema inaendelea kuwajibika katika kutetea na kulinda haki za watoto lakini imesikitishwa na jaribio la kamati hiyo kuingilia mafunzo ya kanisa katoliki kuhusu hadhi ya maisha ya mwanadamu na uhuru wa kuabudu.
Ripoti hiyo pia imependekeza kanisa hilo libadilishe sheria zake kuhusu utoaji mimba na mafunzo ya namna ya kuishi baada ya vijana kubalehe katika shule za kikatoliki ili kuhakikisha haki za watoto na upatikanaji wa huduma za afya zinahakikishwa.
Vatican ambayo ni mwanachama wa mkataba wa umoja wa mataifa wa kulinda haki za watoto uliofikiwa mwaka 1989 ulikubali kuchunguzwa na jopo hilo la wataalam.
Usiri mkubwa umefunika maovu ya muda mrefu.
Tangu mwaka 2001,visa hivyo vya unyanyasaji watoto kingono vilivyoripotiwa kutoka maeneo mbalimbali duniani vimekuwa vikishughulikiwa na kanisa hilo kupitia idara yake ya sheria.
Papa aliyestaafu mwaka jana Benedict wa kumi na sita, alikuwa kiongozi wa kwanza wa kanisa katoliki kuwaomba msamaha wathiriwa wa unyanyasaji huo na kutaka kutovumiliwa kwa maouvu hayo.
Mrithi wake Papa Francis mwezi Desemba alisema kanisa hilo linapaswa kuaibika kwa kuhusika katika udhalilishaji kingono kwa watoto na kuunda jopo maalum la kuchunguza uhalifu huo,kuzuia kuendelea kwake na kuwashughulikia waathiriwa.
Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis
Kamati hiyo ya Umoja wa Mataifa ilisifu hatua hiyo ya Papa Francis lakini ilisema hiyo haitoshi kwani ni wakati uongozi wa kanisa uanzishe mfumo huru wa kushughulikia masuala ya haki za binadaamu kuangazia maovu hayo.
Shirika la kutetea haki za waathiriwa walionyanyaswa kingono na makasisi SNAP limetaka hatua za kisheria sasa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo.
Source: Reuters
0 comments:
Post a Comment