28 December 2013

Kuna watu wanashangaza sana hapa duniani, utawasikia wakisema... "Wanawake ndio sababu ya matatizo yote duniani"

Watu wenye kusema hivyo nakubaliana nao kwa jambo moja, Wazazi wao wa Kike wametaabika miezi tisa, kisha wakajifungua kwa tabu na machungu mazito sana... Kisha wengine wakabahatika kunyonyeshwa na mama zao, kiasi cha kujitambua kuwa wao sasa ni wanaume wa shoka, kumbe masikini wazazi hao hawakujuwa kuwa taabu na mashaka yote yale, mtoto aliyejifungua limekuwa toto jinga na hasidi mkubwa na tena mpumbavu hasiye na adabu wala kujuwa vibaya, kiasi cha kuweza kutamka maneno machafu kama hayo... nasema tena kwa sauti kubwa ili kuweka msisitizo Wenye tabia hiyo MKOME...!

Wanaume wengi wamekuwa ni wakosefu wa adabu, kuwasingizia wanawake kila ovu linalopita hapa duniani, utafikiri kuwa wanawake ndio wameumbwa kwa ajili hiyo... !

Uko majumbani nako kuna mambo, utawasikia wakisema "Muacheni atajijua kwani akiharibika si yeye kila mtu na maisha yake".

Kila mtu na maisha yake vipi, wewe unafikiria mtoto wa jirani akiwa kibaka, mwizi au jambazi, siku akija kukuibia utasema shauri yake na maisha yake?
Je ni sawa kutojali maisha ya wenzentu, kiasi cha kuona mtoto wa jirani akiharibikiwa na kutizama tu, bila kuchuwa hatua zinazofaa? Japo kunyayua kinywa na kutamka kwa kuonya kuwa anachofanya si kizuri? Nasema tena… Wenye tabia hiyo MKOME...!

Na hao majirani nao, wanachangia sana kuharibika kwa jamii, utawasikia wakisema "Wanangu tu tabia zao zinanishinda ya nini nihangaike na toto la mtu".

Haya wewe shindwa na wa kwako, na wajirani mwachie jirani, ila mitaa ikijaa vibaka, Malaya na wavuta bangi tusilalamike maana wa kwako anakushinda, jirani naye wa kwake wanamshinda, mtaa mzima kama si kitongoji kila mzazi anashindwa na wa kwake… Mwishowe wanapatikana vijana wasio na adabu wala nidhamu za kimaisha. Wenye tabia hiyo nanyi MKOME...!

Wazee nao hawapo nyuma, kila kukicha utawasikia "Vijana wa siku hizi hawa, utawaezea wapi".

Ni kweli tutawaezea wapi ili hali tumeshindwa kuangalia mustakabari wa maisha yao tangia wachanga, leo hii tunawasema kuwa eti vijana wa leo tutawaezea wapi!

Kama tutaogopana kwa kuwa tu ni mtoto wa jirani, basi ujuwe na wa kwako pia ataogopwa kukanywa na jirani… Hao watoto zetu uko wanapokwenda kucheza mipira na michezo mingine, ni nani anawaangalia kama si sisi wapiti njia, kama kila mtu atakumbatia wa kwake basi watoto wakiharibika hakuna wa kumlaumu bali sisi wenyewe ambao kila tukiona vijana wakiharibika tunaangalia pembeni na kujifanya kuwa hatuoni kwa kuwa tu anaye haribika si katika watoto zetu au wa ndugu, jamaa au rafiki zetu.

Ndio tunaona kila pembe wacheza kamari sie, walevi sie, wavuta bangi sie, mambo ya kikubwa sie, na kila baya sie.

Je hatukomi tu, tukaanza kuwakanya watoto zetu…! Kama hatuwezi tusilalamike maana tumeshindwa wenyewe kuwalea watoto tulio waangaikia usiku kucha, leo tumejaaliwa watoto tumeshindwa kuwalea kwenye maadili mema…!

Basi na TUKOME SOTE...!

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!