Taarifa za kuwepo kwa nabii huyo anayejulikana kwa jina la Yaspi Bendera, kumefanya baadhi ya wagonjwa kuanza kumiminika katika kanisa lake la Ufunuo kwa Watu Wote lililopo eneo la Yombo Buza-Kipera, Wilaya ya Temeke, wengine wakidaiwa kutoka hospitalini, kwenda kupata ‘uponyaji’.
Lakini serikali imeonya dhidi ya vitendo vya baadhi ya watu kuwaondoa wagonjwa hospitalini na kuwapeleka kwenye maombi, ikisema mtu yeyote anayesababisha wagonjwa kuondolewa hospitalini kwa ajili ya kwenda kufanyiwa maombi atachukuliwa kuwa ni adui namba moja katika jitihada za kupambana na ugonjwa huo na kusisitiza kuwa wagonjwa ni lazima kwanza watimize dozi wanazopewa na wataalamu hospitalini ndipo waendelee na imani zao.
Wakati wataalamu wakisema kuwa ugonjwa huo unatokana na mbu aina ya aedes egypti, Nabii Yaspi anadai kuwa homa ya dengue ni pigo lililoletwa na Mungu kwa watu wasiotaka kumtii.
Nabii huyo alidai kuwa alionyeshwa na Mungu miezi miwili iliyopita kuwa homa ya ugonjwa huo ingeibuka nchini na kwamba itawaathiri zaidi watu wazima kuliko watoto.
Alidai kuwa moyoni ana siri nzito ambayo atamwambia mkuu wa nchi peke yake na iwapo atakosa fursa ya kufanya hivyo, hatamwambia mtu mwingine.
“Nina siri ambayo nataka kumwambia Rais Jakaya Kikwete na tayari nimeshaomba kukutana naye. Kama akikataa sitamwambia mtu mwingine yeyote,” alisema.
Nabii Yasp alitoa madai hayo huku ugonjwa huo ukiwa ushaua watu sita na wengine 600 kuugua katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Shinyanga, Zanzibar na Lindi.
Inadaiwa kuwa mpaka sasa, nabii huyo ameshaponya watu sita kwa kutumia kinywaji cha juisi na maombi.
“Kuna mgonjwa wa dengue alikuja kanisani Jumapili kuombewa akitoka wodini Muhimbili, baada ya maombezi alipona kabisa na sasa ni mzima,” alisema.
Inadaiwa kuwa mgonjwa huyo aliambiwa na nabii anyanyuke akashindwa, lakini baada ya kunyweshwa juisi hiyo na kuombewa aliulizwa kitu gani hawezi kufanya na ambacho angependa kufanya wakati huo, ndipo mgonjwa alijibu kuwa alitaka kutembea, nabii alimwambia “simama utembee”.
Katika hali isiyo kuwa ya kawaida, Emmanuel badala ya kutembea alianza kukimbia kwa furaha akizunguka kanisani. Baada ya tukio hilo, mgonjwa huyo aliambiwa arudi hospitali akawajulishe madaktari kuwa amepona.
Mgonjwa alirudi Hospitali ya Muhimbili kutolewa mpira kama alivyokuwa ameshauriwa na nabii. Siku tano baadaye alikwenda kanisani kumshukuru Mungu, huku akisimulia namna alivyowashawishi wagonjwa wengine wa dengue kwenda kunywa juisi ya muujiza.
Kauli ya Serikali ya Mkoa
Lakini, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amekemea kitendo hicho akisema mtu yeyote anayesababisha wagonjwa watolewe wodini kwa ajili ya kwenda kuombewa, atachukuliwa kuwa adui namba moja dhidi ya jitihada za serikali za kutokomeza ugonjwa wa homa ya dengue.
Sadiki alisema mgonjwa anayetaka kwenda kuombewa aende baada ya kumaliza dozi aliyoandikiwa na siyo kuondoka hospitalini na kuacha dawa.
“Sitaki kuiingilia imani, lakini kumtoa mgonjwa hospitali akaombewe hilo silikubali,” alisema mkuu huyo wa mkoa na kuongeza kuwa baadhi ya watu wameanza kupotosha wananchi kuwa majani ya mipapai yanatibu ugonjwa huo.
Mganga Mkuu Hospitali ya Temeke
Mganga mkuu wa Wilaya ya Temeke, Dk Silvia Mamkwe alisema ni vyema watu wakaheshimu imani zao, lakini siyo sahihi mgonjwa wa homa ya dengue kuacha dawa kwa sababu ya maombi.
Alisema sheria za manispaa zipo wazi kabisa kuhusu taratibu zinazotakiwa kufuatwa kwa mtu anayetaka kumtoa mgonjwa wodini, kwa hiyo ni kosa mgonjwa kuondoka wodini kwenda kuombewa.
Alisema sheria za manispaa zipo wazi kabisa kuhusu taratibu zinazotakiwa kufuatwa kwa mtu anayetaka kumtoa mgonjwa wodini, kwa hiyo ni kosa mgonjwa kuondoka wodini kwenda kuombewa.
0 comments:
Post a Comment