4 May 2014

 Wauza mafuta ya chakula wametakiwa kuyaweka mbali na jua hali Wananchi wakitakiwa kuacha kununua mafuta hayo ikiwa yameanikwa juani ili kujiepusha na athari kubwa kiafya, ikiwemo ugonjwa wa saratani.

Mkaguzi wa Chakula kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TDFA) Kanda ya Kati, Albert Deule alinukuliwa na gazeti  la HabariLeo akiyasema hayo juzi wakati akijibu maswali ya washiriki wa mafunzo kwa wajasiriamali wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Kibaigwa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Deule alisema jua husababisha mafuta kuchacha na hutengeneza sumu na hivyo yakichemshwa wakati wa kupikia, madhara yake ni makubwa mwilini.
Wananchi msinunue bidhaa zilizoanikwa juani, ni hatari kiafya, njia sahihi ni mteja kusema hapana, watu wengi wanapata magonjwa ya tumbo kwa kutumia mafuta yasiyofaa, ni muhimu bidhaa zikawekwa mahali salama wakati zinauzwa,” alisema.

Pia, alisema ni muhimu kwa wajasiriamali kutafuta namna nzuri ya kufungasha mafuta na sio kama sasa, ambapo hata chupa za maji zilizotumika zimekuwa zikitumika kuuzia mafuta.
Alisema chupa nyingine huwa si salama kutokana na kutumika kwa matumizi mengine na ndipo hutumika tena kwa ajili ya kuuzia mafuta.

“Vifungashio ni tatizo kwa wajasiriamali, lakini ni lazima wajali afya za walaji na wateja wahakikishe wanakagua bidhaa muda ulipotengenezwa na muda wa mwisho wa matumizi ya bidhaa hizo,”

Mkaguzi huyo wa chakula alisema ni muhimu wafanyabiashara, wakafuata utaratibu kabla ya kuanza biashara ili kuweza kuzalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa, tofauti na sasa ambapo wengi wanaanzisha biashara ya usindikaji wakiwa hawana mahali maalumu pa kufanyia biashara zao huku mazingira ya biashara, yakiwa hayaridhishi.

Alisema wajasiriamali wa usindikaji ni lazima wazingatie usafi na kama biashara ya kukoboa na kusaga nafaka inaendeshwa bila kuwa na choo, hakuna mbadala, biashara hiyo wataifunga tu.

“Mfanyabiashara asiye na choo, hana msamaha, peleka sokoni bidhaa inayofaa” 

Alisema kisheria shughuli za usindikaji, zinatakiwa kuwa na mtaalamu anayesimamia shughuli zote ili bidhaa zinazozalishwa ziwe bora.

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!