15 April 2013


KWA nini majina yaleyale katika mistari hii? Ni kutokana na kile kinachojiri. Kuna baadhi ya mastaa Bongo ni vigumu kukwepa kuwazungumzia kutokana na drama zao za kila kukicha. Unaweza ukakwepa kuwazungumzia Wema Sepetu, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Khaleed Mohamed ‘TID’ gazetini lakini wakawa wametawala kwenye mitandao ya kijamii. Kwa nini? Ni kwa sababu hawakosi vitimbi. Kama siyo kufumwa wakifanya vitu vya ajabu, basi watakuwa wanagombana.
Uwoya.
Kwa mara nyingine nazungumza nanyi waigizaji wa filamu za nyumbani, Vincent Kigosi ‘Ray The Greatest’ na Irene Pancras Uwoya.
Nianze na wewe Ray. Kama hukumbuki, nitakukumbusha. Alipofariki Steven Kanumba ‘The Great’, nilikuandika hapa. Nikakutahadharisha juu ya anguko lako katika sanaa kwa kuwa mshindani wako wa kibishara na swahiba wako Kanumba alikuwa ameondoka. Sijui kama ulikubaliana na mtanzamo wangu kwa kuwa nilikueleza ni kwa jinsi gani kishindo cha anguko lako kitakavyokuwa kikubwa.
Wiki iliyopita Ray uligeuka gumzo. Kisa? Maadhimisho ya kumbukumbu ya marehemu Kanumba ya mwaka mmoja tangu alipoondoka kwenye uso wa dunia.
Sawa, ulifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kwenda ibadani Kimara, makaburini Kinondoni na katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni, Dar.
Ray.
Dosari ilitokea wapi? Ni pale ulipodaiwa kuifanyia dhihaka siku hiyo kwa kulewa na kushindwa ‘kubalansi’ mambo. Ulipopewa kipaza sauti useme neno juu ya marehemu Kanumba ilishindikana. Kuna wakati ulitamka tusi huku ukimwita mwigizaji Jacob Stephen Mbura ‘JB’ aje jukwaani kuserebuka, ukijisifia kuwa siku hizi umekuwa modo? Ni aibu iliyoje?
Najaribu kueleza ‘situation’ ilivyokuwa mbaya kwa Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity kushindwa kutoa hotuba itakayotoa picha ya wapi sanaa hiyo inakoelekea kama inakua au inadumaa, mwaka mmoja baada ya kuondoka mwigizaji kipenzi cha Watanzania.
Utakumbuka ulipokuwa jukwaani uliulizwa juu wapi walipo akina Wema na Lulu (Elizabeth Michael), ulijibu nini? Nikukumbushe? Ulisema Wema Kafa! Lulu akija Leaders atauawa! Kweli? Majibu gani hayo?
Kuna taarifa kuwa ulishindwa ‘kujikontoo’ kutokana na kulewa kupita maelezo. Pole kaka Ray!
Namgeukia Uwoya. Mama wa mtoto mmoja, Krish. Kupitia kamera za gazeti hili, wiki iliyopita ulijaza ukurasa wa mbele. Ishu ilikuwa ni kunaswa hotelini na Diamond, ikidaiwa kuwa mlilala chumba kimoja kwa takriban saa 10, usiku hadi alasiri.
Ukiwa Makamu Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity ukimsaidia kwa karibu Ray, haukutengeneza picha nzuri mbele ya jamii pana kwa kuwa wewe ni kioo cha jamii.
Uwoya wewe ni mke wa mtu, mchezaji soka wa Rwanda, Hamad Ndikumana ‘Kataut’. Mlikula kiapo mkafunga ndoa kanisani mwaka 2009. Mkapita mabonde na milima. Kitendo cha kuhisiwa, achilia mbali kunaswa kwa kashfa ya usaliti katika ndoa ni jambo baya.
Ona sasa, pamoja na heshima kubwa uliyojijengea katika filamu za Kibongo ndani na nje ya nchi, umeipoteza kwa usiku mmoja na Diamond. Shame! Unakumbuka ulivyopokelewa Rwanda juzikati?
Wote kwa pamoja, narudia maneno yangu niliyowaeleza katika makala yangu hapa mwaka mmoja uliopita. Shule ni muhimu. Wasanii wengi wanaugua USHUKI yaani Upungufu wa Shule Kichwani. Nina wasiwasi kuwa miaka mitano ijayo, tasnia itakuwa mahututi. Muda wa kuweka mikakati mnautumia katika starehe na anasa zisizokuwa za lazima.
Najua maneno yangu yataingilia sikio la kulia na kutokea la kushoto au tuseme ndiyo sikio la kufa halisikii dawa? Badilikeni.
This is for the love of game!
Source global publisher
Reactions:

0 comments:

Post a Comment

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!