12 March 2015


Leo katika kudurusu durusu kwangu, nikakutana na Ayat katika Qur'an ziliyonivutia sana, haya hizi ni kutoka Sura Al- Baqara Ayah ya 237 na Ayah ya 263 na nyingine Surat Ash-Shuura [42]:43 na nyingine ni Suratun Nur [24]:22.

Sura Al- Baqara [2]:237
...Na kusameheana ndiko kulio karibu zaidi na uchamngu. Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.

Sura Al- Baqara [2]:263
Kauli njema na usamehevu ni bora kuliko sadaka inayo fuatiliwa na maudhi. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha na Mpole.

Surat Ash-Shuura [42]:43
Na anaye subiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.

Suratun Nur [24]:22
...Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.

Kilicho nivutia katika ayah hizo ni kitendo cha sisi kusameheana, kumbe kusamehe ni bora zaidi kuliko kulipiza kisasi. Maana kulipiza sio ubaya kama ulivyotendewa lakini kusamehe ni bora zaidi na unapata thawabu kubwa.

Japokuwa mtu amekudhulumu inafaa uitafute haki yako kwa njia zote zile za kisheria ili urudishiwe haki yako. Wala usichoke kufanya hivyo kwani kuachilia haki yako itamfanya mtu huyo awe na ujasiri wa kukudhulumu kwa mara nyingine tena na tena na haswa mtu huyo akiwa si mwenye aqida au tabia nzuri.

Unapodhuliwa kwa namna yoyote ile Uislamu umekupatia njia tatu ya kuliendea suala hilo:
Kulipiza kisasi au kumsamehe na kufanya subra au kumuachia Mwenyezi Mungu.

Hakika ni kuwa kusamehe ni bora, kwani kufanya hivyo kuna faida nyingi nitataja chache zifuatazo:

1: Kusamehewa madhambi. (Q 24:22)
2: Kupandishwa daraja na kuwa miongoni mwa Muhsiniyn (Q 3:133)
3: Kulipwa ujira kutoka kwa MwenyeziMungu (Q 42:40)
4: Kuwa pamoja na MwenyeziMungu, na kulipwa ujira wa kusubiri. (Q 16: 126 - 128)

Licha ya faida hizo ambazo MwenyeziMungu amezitaja kwenye Qur'an, vilevile kuna faida za kisaikolojia pale mtu anapomsamehe yule aliye mkosea, kwa kisaikolojia kumfanyia adui Muisilamu mwenzio hakuwezi kuondoa ubaya, ila nasaha na mawaidha ndio yanayoweza kumbadilisha mja kuwa mja mwema.

MwenyeziMungu kaweka hukumu za kulipiza kisasi, ili tusidhuliane kwa kuona kuwa nikifanya jambo fulani basi nami nitafanyiwa kama ilo.

Watu wengi wanashindwa kuelewa kwamba kushikwa na hasira sana ni dalili ya kutopevuka kiakili. Hata hivyo, tusikereke na watu wanaotukera na kutuudhi mara kwa mara, bali tuwafunike kwa shuka ya amani na upendo na kwa nasaha njema.

Kwa sababu binadamu anapofanyiwa makosa, moyo wake ujaa hamaki na chuki kwa yule aliyemkosea, na hii upelekea akili yake kuweka niya ya kulipiza kisasi, wakati huo huyo ndani ya mwili wake usambaa aina ya kemikali inayotokana na kumwagika kwa nyongo, ndio maana tunapotwa na hasira au maudhi mioyo yetu upata maumivu na hata kuuguwa kwa kipindi kile ulichokasirika.

Hali hii ikiwa inajitokeza mara kwa mara basi mtu mwenye kukasirika anaweza kupata matatizo ya Moyo au vidonda vya tumbo, vilevile anakuwa hana utulivu kwenye nafsi yake na haswa kila anapo muona yule aliyemkosea.

Usipo samehe kuna mengi unayakosa kama nilivyo eleza faida nne hapo juu, Usipo samehe hutopata utulivu wa nafsi, kwa sababu unajirimbikizia machungu ambayo ukupelekea maradhi ya saratani ya akili na kupelekea kuwa na maamuzi yasiofaa na yaliojaa visasi na chuki.

Mifano tunayo ndani ya nafsi zetu wenyewe, ni vipi tunajisikia pale tunapo waona wale walio tukosea, ni vipi tunajisikia tunapokwenda kwenye shughuli mbalimbali, tukajumuika kwa furaha na mara akatoea au wakatokea wale tunao wachukia kwa kuwa tu walitukosea na hatukuwa samehe, je unajihisi vipi ndani ya nafsi yako?

Kiukweli uwa tunahisi taflani na ile furaha tuliyokuwa nayo huyeyuka na nafasi yake uchukuliwa na maumivu ndani ya mioyo yetu. Kiasi cha kutaka hata kuondoka kwenye hizo sherehe au mihaliko.

Lakini ikitokea kuwa tumesamehe, basi hata MwenyeziMungu naye hutusamehe pia na vilevile tunapata utulivu ndani ya nafsi zetu. Na darja zetu hupanda.

Lakini kusamehe kuliko bora ni pale ambapo uwezo wa kulipiza kisasi tunao, lakini tukasamehe, kwa sababu aliyekukosea unamudu kwa kila hali.

Basi tuwe wenye kusameheana sisi kwa sisi...!

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!