11 November 2014

By Kichaa Cha Mwendawazimu Aliyechanganyikiwa

%^&*()+£€?# zenu....! Leo nahisi Kichaa changu kimepanda au sijui kimepandishwa, yaani hata sielewi, kinacho endelea vichwani mwa Wabongo wanaoishi ndani ya nchi ya Wachawi Giningi, heri mie Mwendawazimu Kichaa Aliyechanganyikiwa, kwa sababu hakuna anayeweza kuniangalia mara mbili, zaidi ya wale watoto wanaopenda kunitania na wengine wakifikiria kuwa eti nimesoma sana mpaka vitabu vikiniona vinachakaa vyenyewe, ndio akili zikaelewa saaaana mpaka nikawa Mwendawazimu Aliyechanganyikiwa.

Hivi hawa wenye akili sana zilizopitiliza mpaka wakawa Wachawi, uwa wanafikiria nini kwenye vichwa vyao, hivi hawajui kuwa wale wenye akili robo ndio walio wachaguwa kuwa pale walipo? Eti nasikia kuwa baadhi ya vyama vya Kichawi vimeamua kuungana ili kukichangia na kukigomea chama Kikuu cha Wachawi.

Ah ah ah ah ah...! Kaaazi kweli kweli...! Wachawi awa awa si ndio kwenye Bunge lao la Wachawi, wamejipandishia masurufu kiasi cha kutisha, kama kweli hawa Wachawi wapo kule kutetea Misukule na Mandondocha, wangekuwa wanawashirikisha ndondocha na misukule wote kabla ya maamuzi yao. Lakini ni pale tu, Chama Kuu la Wachawi, likitumia uchawi wake mkuu, ndio utawaona Wanga na Wachawi wengine wakipiga kelele na kucheza mahepe, wakitaka kuwashirikisha ndondocha na misukule.

Nao Mandondocha na Misukule kwa kulewa na Uchawi na Urozi wa vyama vyao vya Kichawi wanawashabikia, wamelewa dawa za kuondoa akili a.k.a propaganda kiasi ya kwamba hawaoni hawasikii.  Ushabiki umekuwa mkubwa kiasi ya kwamba hawaoni wala hawasikii tena. Wanatamanishwa kila leo, lakini masikini hakuna wanacho kipata, wanaomba, wanatamani, mwisho tamaa na maombi yanasahaulika.

Wachawi wote, lao moja, sioni hata Mchawi mmoja mwenye afadhali. Sasa hivi kila kona unayokwenda Misukule na Mandondocha wanalalamika hali ngumu! Utamkuta mtu jicho limemtoka  kama yai la Mbuni "Hatukubali. Ngoja uchaguzi uje. Mchawi huyu sasa basi. Mimi kura yangu kwa naniu tu safari hii. Eeh, ndio! Mffvyyyy! Kshxnz$!!! kabisa! Blah...blah...blah...!"

 Ukiwa Mwendawazimu Aliyechanganyikiwa kama mimi ndio unafaidi. Miye sina Mchawi hata mmoja ninaye mpenda. Usiniulize, kwa sababu Kichaa haulizwi, ukitaka kuwauliza bora uwaulize hao hao Misukule wenzio au waulize Mandondocha, ndio wenye uwezo, japokuwa hawajui kuwa wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko ya maisha yao.

Nauliza tu wale wanaojidai wana hasira, hasira hizo ni za kweli au Vifuko vikitolewa tu, "Thalamaleku, uku wengine bwana athifiwe nyiiingi...!"

Wengi wanashangaa haswa lengo la haya ninayoyasema ni nini, wacha niwaambie kuwa sina lengo lolote, kwanza toka lini Mwendawazimu Aliyechanganyikiwa akawa na malengo? Hayo malengo muwe nayo nyinyi wenye Akili na Wachawi wenu walio wafanya nyinyi kuwa Mandondocha na Misukule, mnalishwa pumba sawa! Mkilishwa Makapi sawa! Ila mkimwa matumbo, mkienda uko mnapo paita Sipiti-ni-hatari, I mean Sipatihali, Oops nina maanisha Hosipitali, ndio hosipitali, mnakumbana na maudhi mengine na kukatishana tamaa.

Hakuna Mafusho ya kufukisha wala, hirizi za kuwavika msiumwe magonjwa ya kuhara, matumbo yanasokota kwa kula pumba kavu, sasa unashangaa nini, kwani tangu lini, ndondocha au msukule akatibiwa?

Basi wacha niwaambie na nina uhakika kabisa Wandondocha na Misukule wote wamekwisha hukumiwa kifo tayari...! Ndio kwani hujui kuwa Bongoland, hukumu ya kifo inafanyakazi!?
Ndio inafanyakazi japokuwa si kwenye mahakama rasmi, lakini Wachawi wakishirikiana na Wanga wamesha wahukumu... Japokuwa si kile kifo cha kunyongwa hadi kufa kwa kuning'inizwa kambani au kupigwa risasi lakini cha moto wanakiona...! Maana wanakufa taratibu wakijiona na machozi yenda na maji hakuna wa kuyaona.

Tena siku hizi wachawi hawa wenye akili sana wamehamia Mbinguniiii kwa taarifa yenu. Maana hata kujenga wanajenga uko uko mbinguni, uku ardhini wanakuja tu, siku za Ijumaa na Jumapili, ili nao waonekane onekane, ili hali wanajuwa kuwa Mungu wao na Mungu wa Mandondocha ni tofauti.

Uko Sipiti-ni-hatari, I mean sipitali wanaotibiwa ni Wanga na Wachawi wenye kujiweza kidogo, kwa sababu, wao ndio Wabia wa nchi hii. Ila wale Manguli wa Uchawi walio na Ubia katika nchi hii... Unashangaa nini, ndio kwani hujui kuwa nnji hii imikwisha uzwa, shauri yako... Basi Wachawi wakipata faida, upeleka kuweka pesa zao uko mbinguni Uswisi. Wakitaka kufanya shopingi za wajukuu zao wanao wandaa kuja kutawala Ndondocha, wanakwenda zao mbinguni Dubai, mapumziko mbinguni Ufaransa, wakiumwa haoooo wenda zao mbingu ndogo India, ila Wachawi wengi wanaona kuwa mbingu ndogo India siku hizi hata baadhi ya Mandondocha wanakwenda, basi tena wamebadirisha, wenda zao Mbingu ya Londoni na wengini mbinguni Marikani.

Lakini ni ajabu sana Wachawi hawa, matibabu, shopingi, mapumziko yooooote yanafanyika Mbinguni, basi na mkifa Mzikwe uko uko Mbinguni, muwaambie jamaa zenu kabisaaaa, maana Bongoland sio Makaburini.

Ndioo... Eeeeh, Haiwezekani Mtumie mapesa yoote kwenye kujifaharisha uko Mbinguni, siku mkikata roho tu, mnaletwa duniani (Bongoland) kuja Kuzikwa, kwani mmesikia kuwa Bongoland ndio Makaburini, kwanini msizikwe uko uko Mbinguni kwenu!?

0 comments:

Post a Comment

.

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!