Mwandishi Wetu.
SHERIA ya Filamu ya mwaka 1976 nambari 4 inaipa mamlaka Bodi ya Ukaguzi wa filamu na Michezo ya Kuigiza kukagua na kutoa madaraja kwa filamu zinazozalishwa nchini Tanzania, lakini kwa sasa kuna hali ya sintofahamu kwa taasisi hiyo yenye mamlaka ya kukagua filamu hizo ambayo ipo kisheria.
Sitaki kuingia ndani sana kuongelea sheria hiyo kwa sababu ipo wazi na wenye wajibu wa kutoa elimu hiyo kwa watayarishaji na wasmbazaji wa filamu ni Bodi husika, lakini pengine kuna baadhi ya watayarishaji na wasanii wanyonge wasio na majina wanaanza kuhisi kuwa Bodi hiyo ipo kwa ajili ya kukandamiza wanyonge na si wafanyabiashara wakubwa wenye nguvu kama ilivyo sasa.
Siku za nyuma Bodi hiyo iliwahi kusimamisha filamu ya Shoga kwa sababu ilikuwa ikitaka kuingia sokoni kabla ya kukaguliwa jambo ambalo ni kinyume cha sheria, uliibuka mtafaruku na hatimaye baadaye msambazaji wa filamu hiyo alitii na kuwakilisha filamu hiyo na kukaguliwa na kufanyiwa mabadiliko ikiwa ni pamoja na jina na baadhi ya vipande kutolewa, filamu hiyo ikabatizwa jina la Shoga Yangu.
Msambazaji wa filamu hiyo ambaye ni Al Riyamy Production baada ya kupata ushauri aliamua pia kupeleka kazi zake nyingine kwa ajili ya kukaguliwa kati ya filamu hizo tano zilipata Daraja la R maana yake kuwa hazifai kuingia sokoni, filamu zilizokumbwa na dhahama hiyo ni Iny’e, Iny’e Plus, Iny’e Gwedegwede, Iny’e Mdebwede na Mtoto wa Mama.
Hizi filamu zilifungiwa baada ya Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya kuigiza kitalaam kuona zina matatizo ya kimaadili ikiwa udhalilishaji kwa wanawake na kuchochea mambo ya kishoga. Filamu iliyoashiria ushoga ilikuwa ni Mtoto wa Mama pengine filamu ya Shoga nayo jina liliwaponza.
Kwa zoezi hilo kila mtu mpenda maadili aliona wazi kuwa sasa Bodi imekusudia kulinda maadili na kuhakikisha kuwa filamu zinazotoka zinakuwa ni bora na kazi imeanza na moto huo hautazima na kuanzia hapo watayarishaji walishituka na kuanza kuona umuhimu wa kufuata sheria.
Hadi leo mwathirika mkubwa ni Al Riyamy Production tunasema hivyo kwani huyu aliwekwa hadharani lakini hawa wengine hatujui kama wapo, lakini mazingira yanayozua utata kuhusu ukaguzi wa filamu hizi ni pale tunapoona sheria hiyo haizigusi filamu zinazotolewa na wasanii wenye majina huku wakiwa ndio wenye kuifikia jamii kwa urahisi zaidi.
Wasanii hao nyota tunasema kuwa wanaifikia jamii kwa urahisi kwa sababu wasambazaji wanapotoa filamu zao matangazo ya kuzitangaza filamu hizo kwa kutumia kila njia yoyote ili wanunuzi waweze kununua kazi hizo ikiwa ikitumia kwa kutumia magazeti, televisheni na mitandao ya Kijamii hapo kwa asilimia kubwa taarifa zinawafikia.
Mfano mzuri ni filamu iliyotoka hivi karibuni ya Ndoa Yangu ambayo imeandikwa au kuwekwa alama ya alama ya PG 18 sijui hili ndilo daraja jipya linalotolewa na Bodi hivi sasa, lakini pia kuna utata kuhusu daraja hilo kwani filamu ikiandikwa alama PG (Parental Guidance) Daraja hili haliambatani na namba kwa maana ya umri, jambo linalotushangaza kuona PG ikiambatana na 18.
Kwa wenzetu waliotutangulia ukiona filamu imewekwa alama ya PG (Parental Guidance) ni Daraja la chini sana ni filamu zinazoweza kutazamwa na watoto wale waliopo katika uangalizi ikiwa Shule za chekechea au mzazi mlezi ambaye anatumia filamu hizo kama kitu cha kumbembelezea ili mtoto aweze kufurahia kwa kifupi Daraja hili halina madhara. Je, katika filamu ya Ndoa Yangu hali ipo hivyo?
Kama filamu hiyo imekaguliwa basi ni fedheha kwa waliokagua na kutoa daraja hilo, kwa hili nazidi kukata tamaa kuwa tasnia filamu Tanzania kuwa inapotea njia. Huu ni utapeli kama si kutojua matumizi sahihi ya alama hizo za kimataifa ambazo sina hakika kama ni alama iliyowekwa na Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza.
Alama hiyo inajichanganya sana kama nilivyosema awali. Daraja la PG linalotolewa katika katika filamu za nje ni la chini likihusu filamu zisizo na ukomavu wa akili, huku umri wa 18 kwa Tanzania ikimananisha ni mtu mzima hapo ndio penye mkanganyiko mkubwa kuhusu alama hiyo kwa wanajua mambo ya filamu.
Lakini katika kumbukumbu hatuna hakika kama filamu za hawa tunaowaita wasanii nyota kama zinakaguliwa pamoja kuwafikia Watanzania kwa wingi zaidi kwa mfano filamu ya Ndoa Yangu sitaki hata kuongelea kilichomo ndani zaidi tu ya kuhoji sheria hiyo ya mwaka 1976 namba 4 ipo kwa ajili ya nani?
Filamu ya Shoga kabla ya kuingia sokoni ilisimamishwa na kuzua balaa kwa msambazaji kufungiwa filamu zake tano ambazo inawezekana zikawa zina matukio yanayojiri mitaani, lakini kuna matukio kama ya kuonekana mtu akijichua ni kitu cha kawaida tu wala si tatizo ruksa kwa sababu ni filamu iliyotolewa na kampuni kubwa na wasanii nyota.
Maadili yapi yanayoongelewa katika tasnia ya filamu nchini? Tafiti zinaonyesha kuwa filamu mpya inapotoka wateja wakubwa ni wa ‘vibanda umiza’ ambao wanaoonyesha filamu hizo pasipo kujali umri wa watazamaji. Je, kwa kuweka alama ya PG 18 tutaweza kuzuia watoto wa ‘Walala hoi’ ambao ndio sehemu yao ya faraja katika mabanda hayo?
Hali hiyo ya kuwabana baadhi ya watayarishaji itadumu kwa hadi lini?
Ukitembelea maduka mengi hadi leo hii, ni filamu moja tu ambayo imeingia sokoni ikiwa na alama ya Bodi ya Ukaguzi na Michezo ya kuigiza ambayo ni filamu ya Chungu inamaana ndio filamu pekee iliyokaguliwa kwa mwaka huu?
Katika hali kama hiyo hujenga imani mbaya na watendaji na kuonekana kama ni watu wanaonyenyekea baadhi ya wasambazaji tena wenye nguvu katika tasnia ya filamu nchini, leo hii kampuni kama ya Al Riyamy inapata picha gani kuhusu sheria ya upendeleo huo?
Kwa mantiki nyingine Bodi inafanya kazi na wale tu wanaojua umuhimu wa sheria lakini kwa wakaidi ndio marafiki zao, Bodi haiwezi kufanya kazi kwa kusubiri matamko kwa kufanya hivyo inaingia katika kuwagawa wasanii na wadau wa filamu ambao wanaamini kuwa mwenye nacho huongezewa kwa hata akivunja sheria bado atabebwa tu ili afanye biashara kwa maslahi yake huku jamii ikilalamikia uvunjifu wa maadili.
Wauzaji wanalalamikia Serikali wakidai kuwa suala la uharamia limekuwa kubwa kwa sababu hakuna mwongozo kuhusu nakala halali ya filamu inafananaje, kwani kila msambazaji ana alama zake huku kampuni kama Steps Entertainment ikilalamikiwa kwa kutoa filamu katika aina mbili kwa wakati mmoja yaani ya 2,000/ na 1,000/ kwa wakati huo huo.
Ni vyema sheria ifanye kazi bila kuangalia sura ya mtu kwani ni wazi kuwa tabia hiyo ikiendelea kuivunja si rahisi pengine watu waanza kuhisi kuwa ukisema Shoga ni tatizo zaidi kuliko kitu kingine chochote, filamu nyingi zinazoongoza kwa matangazo zikitangazwa ili zinunuliwe zimejaa uvunjifu wa maadili kuliko zisizo na matangazo na Bodi ‘haioni.’
Inawezekana Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam Idd Azzan alikuwa sahihi alipokuwa akichangia katika Bajeti ya Bunge Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwa kusema kuwa Bodi ya filamu imelala usingizi mzito akitaka iamke kwani inaonyesha kuwa wale wanaowapinga ndio marafiki zao kuliko wanaotii na kuifuata sheria.
Chanzo gazeti la Raia Mwema.
0 comments:
Post a Comment