Waandishi watamani leseni za fani yao |
BAADHI ya waandishi wa habari mkoani Morogoro, wamependekeza kuwa Tasnia ya Habari Nchini, ianzishe bodi ya usimamizi wa maadili ya waandishi wa habari, kama katika taaluma zingine, ili kudhibiti mmomonyoko wa maadili ya fani hiyo. Hatua hiyo inafuatia kukithiri kwa vitendo vya mmomoyoko wa maadaili katika tasnia hiyo licha ya kuwepo kwa jitihada za kutoa mafunzo na miongozo mingi inayotolewa na taasisi mbalimbali likiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT). Wakizungumza katika semina ya siku tatu ya maadili ya waandishi wa habari mkoani Morogoro , waandishi hao walisema kuna haja ya kuwa na bodi ambayo moja ya ma jukumu yake ni kutoa leseni kwa waandishi wa habari na kudhibiti mienendo ya waandishi wa habari. Mmoja wa washiriki wa semina hiyo, Nikson Mkilanya, ambaye ni mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Star na Redio Free Africa, alisema ikiwa waandishi wenye sifa watapatiwa leseni, itakuwa ni rahisi kuwadhibiti wasiokuwa waandishi ambao wamekuwa wakifanyakazi kama wanahabari wengine, pasipo kudhibitiwa. Mkilanya alisisitiza kuwa hatua hiyo itapunguza wimbi la makanjanja na kuimarisha heshima ya taaluma hiyo. Mtoa mada katika semina hiyo, Juma Thomas, ambaye ni mwandishi wa habari na wakili wa kujitegemea, alisema hoja hiyo ni ya msingi na kupendekeza kuwa waandishi wa habari watumie fursa ya kutoa maoni kuhusu katiba mpya, ili sheria iliyopo iboreshwe. Thomas alisisitiza kuwa waandishi wa habari wamekuwa katika mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa sheria zinazokandamiza uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kupata na kutoa habari, zinaondolewa na kwa mantiki hiyo lazima wafanye hivyo katika kushughulikia suala la leseni zao. Alisema wadau wa tasnia ya habari wamekuwa wakihangaika ili kuhakikisha kuwa mswada wa mabaoresho ya sheria kandamizi unafikishwa bungeni lakini imeshindikana kwa sababu zisizofahamika. Waandishi wengine walipendekeza kuwa MCT inaweza kubeba jukumu la utoaji leseni na kuendelea kusimamia maadili ya waandishi wa habari nchini. Tume iliyoundwa na nchi zisizofungamana na upande wowote mwaka 1980 kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni ( UNESCO) ilitoa mapendekezo ya kupinga waandishi wa habari kuwa na leseni kama ilivyo kwa tasnia zingine kwa madai kuwa hatua hiyo inakwenda kinyume na haki za binadamu za kupata na kutoa habari. Mwenyekiti mstaafu wa Moropc, Bonventure Mtalimbo, alisema kuwa zoezi la utoaji wa vitambulisho vya waandishi wa habari (press card) ambalo limekuwa likifanywa na Idara ya Habari Maelezo kama mbadala ya leseni limeonekana kukwama kutokana na utaratibu mbovu uliopo. Alisema kuwa vitambulisho hivyo vimekuwa vikichelwa kutolewa na ukomo wake wa mwaka mmoja umekuwa ukitafisiriwa kuwa ni aina ya biashara ambayo hufanywa na idara hiyo huku idadi ya wanaovitapa ikizidim kupungua kila mwaka. Gazeti la mwananchi Venance George, Morogoro |
0 comments:
Post a Comment