Sheikh Farid Hadi Ahmed
Baada ya watanzania Visiwani kutokukubaliana na katiba iliyopo hasa juu ya mustakabali wa Muuangano,hali iliyopeleka kutokea na machafuko visiwani humo,kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho ya Visiwani Zanzibar Sheikh Farid Hadi Ahmed,amefanya mahojiano na mwandishi wa gazeti la Jamuhuri bwana Manyerere Jackson.
Katika mahojiano hayo shekhe Farid amesikitishwa na kitendo cha serikali ya Tanganyika kuunga'ang'ania mji wa Dar es Salaam huku ikiwa inajua kuwa mji huo upo ndani ya visiwani hivyo kwa maili kumi huku akisisitiza kuwa mikataba inayoonyesha mji huo upo ndani wa visiwa hivyo ipo.
Ameeleza pia lengo kuu la mihadhara waliyokuwa wakiifanya,si kuleta fujo,bali nikutaka kuwaelimisha wananchi juu ya mustakabali wa muungano na katiba kwa ujumla.
Yafuatayo ni mahojiano ya mwandishi Manyerere na kiongozi wa wanajumuiya ya UAMSHO Shekh Farid
JAMHURI: Ni nini chanzo cha vurugu za Mei 26?
Sheikh Farid: Kilichotokea hapa kwa muda mrefu, japo inasikika Jumuiya ya Uamsho ndiyo inayofanya mihadhara, lakini ni Umoja na Jumuiya za Kiislamu ambazo zimekuwa zinaendesha mihadhara. Tumefanya mihadhara zaidi ya mia moja hadi sasa – mikutano zaidi ya mia pamoja na makongamano tofauti. Na lengo zaidi hapo awali lilikuwa ni kuwaelimisha watu kujua Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kuona ni jinsi gani inawabana Wanzibari na haijawapa ile haki yao ya kuujadili Muungano.
Na baada ya hapo kilichokuwa kinazungumzwa zaidi ni kuwaelimisha wananchi kujua haki yao kujua mustakabali wa nchi yao na umuhimu wa kuuhoji Muungano au kuujua Muungano. Wazanzibari wao kama washirika na Watanganyika wana haki ya kuuhoji Muungano. Sasa hii mihadhara imeendelea kwa muda mrefu na ilikuwa inakwenda misafara ya mbali mingine hadi shamba. Na ilikuwa misafara mikubwa inaweza ikabeba magari mia mbili, mia mbili na zaidi, kuna mapikipiki, watu wanakwenda wanarudi kwa usalama wala hakuna tabu na matatizo yoyote. Hayo yote ndiyo kwa jumla yamefanyika.
Sasa kilichojitokeza hivi karibuni ni kuwa lilifanyika kongamano. Katikati ya lile kongamano watu waliamua kutembea, kama ni matembezi tu lakini si maandamano hasa. Maandamano ni kitu ambacho kimeandaliwa, kina slogan yake, kina ujumbe, kinaenda maeneo maalumu kufikisha ujumbe maalumu. Haikuwa hivyo.
JAMHURI: Je, Polisi walivamia?
Sheikh Farid: Polisi hawakuvamia, hawakuwahi kuvamia. Na walipokuja kwa kweli walikuja matembezi yameanza kutoka maeneo ya Lumumba. Watu wote wameacha baiskeli zao, vifaa vyao palepale na walinzi walibaki eneo lile. Watu wametoka wametembea mpaka hapa Michenzani, katika roundabout, wameshuka chini mpaka maeneo ya Kariakoo. Kwa hiyo watu wakaenda moja kwa moja wakarudi kwenye kile kiwanja walichoanzia. Wakarudi palepale wakaaa kitako. Wakawa wanaendelea na shughuli zao. Wakazungumza, wakazungumza mpaka wakamaliza. Walipomaliza kuzungumza wakatawanyika wakaenda majumbani mwao salama salmini.
Nashangaa sasa alipokuja Waziri, Jeshi la Polisi wamemdanganya. Na alipokuja IGP wamemdanganya wamemwambia uongo. Wanamwambia kuwa Jeshi la Polisi limejaribu kuzima fujo, lakini si kweli. Ni uongo huo. CD zipo zinauzwa kila pahali. Wazi kabisa. Zinaonyesha maandamano kitu mbali, na zile fujo kitu mbali kabisa. Hayo matembezi kitu mbali na hizo fujo kitu mbali kabisa.
JAMHURI: Nini chanzo kilichosababisha fujo?
Sheikh Farid: Fujo ilisababishwa na Jeshi la Polisi kukosa utaratibu, kuchukua mazoea yale yale ya uhuni na mabavu. Ndicho kilichofanyika kwa sababu kati ya mmoja wa watu waliohudhuria pale kwenye viwanja palipokuwa na mdahalo ni Maalim Musa Juma, yeye ni mmoja katika wahadhiri wala si kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho, lakini ni mwalimu ambaye anahadhiri, anafundisha. Sasa siku ile yeye alikuwa si mzungumzaji, alikuwa mkaribishaji wa wazungumzaji. Walichokifanya wakati wa majira ya saa moja na kidogo usiku, yumo msikitini mwake anasomesha, alikwenda mtu ana shida naye.
Alipomwita, kutoka nje kuwafuata wale watu wakamkamata kwenye kiuno, na wengine watano wamekuja wamemzoa wamemshindilia kwenye gari wakampeleka kituo cha Polisi. Wale vijana waliokuwa pale – wanafunzi na watu ambao wanampenda, na sasa kimekuwa kitu sensitive kwa sheikh kumdharau. Sasa hii dharau iliyofanyika, wananchi hawajakubali kwa hiyo wakaanza kupigiana simu wote kwamba Sheikh wetu kakamatwa, twendeni tukamdai kwanini kakamatwa, na tujue. Kama kumchukulia dhamana tumchukulie.
JAMHURI: Lipi jina sahihi la Jumuiya hii? Ni Uamsho au Muamsho?
Sheikh Farid: Hizi harakati zinazoendelea hapa nchini (Zanzibar) zinafanywa na Umoja wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu. Ndiyo wanaofanya hizi harakati zote. Isipokuwa katika utaratibu wa mambo ya mihadhara, Jumuiya pekee ina uzoefu mkubwa kwenye mihadhara ni Jumuiya ya Uamsho.
JAMHURI: Taasisi ya kidini kwanini ijikite kwenye siasa?
Sheikh Farid: Hakuna tatizo lolote. Hakuna tatizo kikatiba, hakuna tatizo kidini yetu, hakuna tatizo kimtazamo sahihi wa wanasiasa. Kote hakuna tatizo. Mtazamo sahihi wa wanasiasa. Tumchukue Rais wetu wa hapa Zanzibar, Mheshimiwa Jumbe ameandika kitabu na kuna sura maalumu anaita “Dini na Siasa”. Kaeleza mengi. Kaeleza jinsi watu wengine walivyo katika dini zao, lakini akaelezea ama upande wa Uislamu huwezi kutenganisha dini na siasa. Hilo moja. Basi kama watu wanajua wanasiasa, huyu mwanasiasa anatamka kwenye kinywa chake. Alikuwa Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania. Alikuwa pia Makamu wa Mwenyekiti wa CCM na kaeleza wazi kabisa kwenye Uislamu huwezi kutenganisha na siasa.
Ukija kwenye Koran, Uislamu unahesabu kuwa dini ni mfumo kamili wa maisha ya mwanadamu, ikiwamo sehemu ndogo inayoitwa “siasa”. Siasa kwenye Uislamu au kwenye lugha ya Kiarabu, neno hilo hilo siasa kama lilivyo, maana yake ni “uongozi”, kwa hiyo uongozi ni sehemu ndogo, ni mlango katika maisha ya mwanadamu au katika dini ya Kiislamu. Kwa hiyo sisi kuzungumza siasa ni sahihi kabisa.
JAMHURI: Nyuma ya Uamsho kuna msukumo wa kisiasa?
Sheikh Farid: Uamsho haina uhusiano na CUF. Hili suala limeanza ilipokuja hii rasimu ya Katiba, ilipokuja kama rasimu, Serikali nzima iliikataa, Wazanzibari waliikataa wakaona wamedharauliwa. Iliporudi ikaja na dharau nyingine, badala ya kuletwa kama rasimu ikaletwa kuwa ni sheria sasa…kinguvu. Unaposema sheria maana yake ni nguvu, utake usitake. Ikaletwa kama sheria na ilikuwa iletwe kama rasimu. Hilo tatizo la mwanzo. Tatizo la pili, ndani ya rasimu ile kama alivyosema Mheshimiwa Kikwete mwenyewe wakati anazindua Tume, hakuna mjadala wa Muungano mle ndani yake, ni kwenda mbele tu kuuboresha, lakini suala la kutazama mustakabali wa Zanzibar je, inafaidika na Muungano? Hilo hakuna. Imeshapita miaka 48 na hawajawahi kuulizwa huko nyuma. Sasa sisi hapa ndipo tulipoona kuna haja ya kuulizwa, na njia ya kufanya hivyo ni kupitia kura ya maoni.
JAMHURI: Kuna umuhimu wa kuwapo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?
Sheikh Farid: Sisi tunachotaka ni kura ya maoni. Wazanzibari waseme wenyewe. Hakuna mtu amepewa kibali cha kumsemea mtu. Hakuna Mtanganyika wala Mzanzibari. Kila mtu aseme mwenyewe na hiyo ndiyo demokrasia, kwa hiyo sisi kama Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu tunasema iitwe kura ya maoni. Nisiseme mie, mie nitasema kwenye karatasi. Kila Mzanzibari atasema kwenye karatasi. Kura ya maoni ni nyepesi tu.
JAMHURI: Mbona hamjasikika mkilaani kuchomwa makanisa? Mnaunga mkono kitendo hicho?
Sheikh Farid: Tumeshatoa taarifa nyingi sana. Tatizo unajua hakuna uadilifu kwenye uandishi wa habari. Hakuna uadilifu hata kwenye hii TV yetu iliyopo hapa (ZBC), hata redio zilizoko hapa hakuna uadilifu bwana. Hii ni kwa mtu anachukia kitu anakuwa si mwadilifu. Na haya ndiyo yanayosababisha matatizo kama haya kuzuka. Mtu unamnyima haki yake anafika mahali hawezi kustahamili. Kwa hiyo sisi kiufupi tunalaani vibaya sana suala zima la kuchoma makanisa, dini haisemi hivyo.
Si dini yetu wala si nyingineyo, haisemi hivyo. Lakini tunashangazwa vilevile, tumechoma makanisa, sisi ameuliwa imam ndani ya msikiti na Jeshi la Polisi…ameuliwa imam ndani ya msikiti, huko Mwembechai kwenu huko Dar es Salaam ameuliwa Muislamu ndani ya msikiti. Acha kuchoma makanisa. Sisi tunalaani uvunjifu wa amani wa aina yoyote – ikiwa wa ubaguzi wa kidini wa kuchoma makanisa, ikiwa wa kuwahujumu watu, tukubali haya si mafunzo maana hata kwenye nyumba yangu wamekuja wamehujumu ndani, wamepiga mabomu ndani ya nyumba, wamevunja mlango.
JAMHURI: Mambo gani ambayo Zanzibar haitendewi haki ndani ya Muungano?
Sheikh Farid: Ni mamlaka kamili ya kimaamuzi ya kimataifa, ya ndani na nje ya nchi. Hiki ndicho tunachokosa Zanzibar. Wanaita Sovereignty, Zanzibar inakosa sovereign yake kwa hiyo tunataka sovereign state. Kama ni Zanzibar iheshimike, kama ni Rais wa Zanzibar aheshimike, Serikali ya Zanzibar iheshimike ndani na nje ya nchi. Iwe na mamlaka kamili. Na wao wenyewe (Wazanzibari) wataona utaratibu nini watafanya. Kwa hiyo wananchi waulizwe, chepesi tu hakina tabu. Si waliulizwa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hakupigwa mtu?
JAMHURI: Marekani majimbo yale ni nchi – ni Muungano, mbona majimbo hayana mamlaka kamili kama nchi?
Sheikh Farid: Mbona upo muungano tofauti na huo. Kama Umoja wa Ulaya si upo? Upo vipi? Katika Umoja wa Mataifa si kila nchi ina kiti?
JAMHURI: Huo si muungano ni kama jumuiya tu.
Sheikh Farid: Huo ni muungano, si wameungana katika vitu maalumu? Wamarekani wameamua wao vile. Sisi tumeamua hivi. Wao hatuwasemei. Sie tunaamua tunachotaka sie. Na sisi hawezi kutulazimisha mtu tuamue kwa akili za Kimarekani. Wamarekani wataamua wao wenyewe Kimarekani, haki za Kizanzibari zitaamuliwa Kizanzibari-Zanzibari.
JAMHURI: Ungependa Muungano wa uwe wa namna gani?
Sheikh Farid: Mie ninachosema ule mchakato wa Katiba imekuwa sawa na kumchukua ng’ombe na gari ya ng’ombe halafu ng’ombe ukamweka nyuma gari ya ng’ombe ukaweka mbele. Au mashine ukaweka nyuma, gari ukaweka mbele. Sijui itakwenda vipi. Sasa tunashangaa, watu wataalamu wana akili lakini inaonyesha akili zao zimefika mahali wanatuona sisi wapumbavu. Sisi bwana tunasema ilivyo kitu kinachowafungamanisha Wazanzibari na Watanganyika ni Muungano. Ninyi mnataka kujadili Katiba ya Muungano, hili tatizo la Muungano kwanini msilizungumze mwanzo? Hili la kuzungumza mwanzo. Kwanza, lizungumzwe hili kwanza mpaka likae sawasawa halafu ndiyo tuzungumze Katiba.
Sasa unasema mimi na wewe tunataka kufanya biashara njoo tufunge mkataba mimi na wewe. Si tuzungumze tukubaliane kwanza halafu ndiyo tuandike mkataba kwa sababu Katiba ndiyo umefunga kila kitu. Kitu kinachotufungamanisha tukizungumze mwanzo. Wananchi wapewe fursa wazungumze mwanzo. Watu wanapewa fursa hizo wasiokuwa na nchi mwanzo…hii ni nchi. Hii ni nchi. Ilikuwa ni nchi tena kubwa mpaka Dar es Salaam yote ilikuwa yetu ile, tena mikataba ipo ya kimataifa ya kuonyesha Dar es Salaam yote ile ni yetu sisi. Na kuingia ndani huko maili 10.
JAMHURI: Je, mtaidai Dar es Salaam?
Sheikh Farid: Hatuna shida nayo hiyo. Tutakuachieni. Sisi watu wakarimu sana sie. Tutawaachieni. Nashangaa nyie tu hizi kilomita za mraba ngapi zinakushughulisheni nyie wakati mna mapori tele kule juu, na mna ardhi ya kwenda na kurudi, mashamba ya kwenda na kurudi mnang’ang’ania hiki tu!
JAMHURI: Muungano ukivunjika, nini hatima ya Wazanzibari wanaoishi/waliowekeza Bara?
Sheikh Farid: Jawabu moja, wewe huwajui Watanzania wanaofanya biashara Kenya? Uganda? Hatima yao ipo vipi? Sasa ninyi inaonyesha kuna watu wana fikra mbovu katika vichwa wanaona maana yake tukiwa hivi (tukitengana) tutakuwa maadui, hata! Udugu lazima utabakia. Tumeoa kule. Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar usingizi wake (mkewe) ni wa kule (Bara) au hujui wewe? Hatuwezi kuachana bwana, watu watabakia, mapenzi yapo, undugu upo, ujirani mwema kabisa, waliokuwapo hapa Watanganyika watabakia, Wakristo hapa watabakia, itakuwa kila kitu kina utaratibu. Si maana yake kwamba mmetengana muwadhulumu wale ndugu zenu (walio Bara). Mkiwadhulumu sawa! Sisi kawaida yetu hatuko hivyo.
CHANZO:swahilivillah blog/Mzalendo.net/habari
CHANZO:swahilivillah blog/Mzalendo.net/habari
0 comments:
Post a Comment