16 July 2014


Leo nilikuwa nimekaa peke yangu barazani, nikitafakari hali ya maisha kiujumla, mawazo yakanichukuwa na kunipeleka mbali kiasi, yaani miaka michacahe iliyopita, si miaka mingi sana ni kiasi cha miaka thelathini mpaka arubaini iliyopita, enzi zile kabla hizi simu za mkononi hazijaingia uku kwetu Bongoland.

Enzi zile kutembeleana ilikuwa ni jambo la kawaida sana na tena wakati mwingine bila hata ya taarifa, waweza kumshtukia aidha rafikio au nduguyo toka mkoani amekuja na mabegi na vikapu vyake vya vyakula, kaja kukujulia hali.

Hali hii ilikuwa ni kawaida sana na kama imetokea ujaonana na rafikio au nduguyo kama si jamaa yako basi aidha utamwandikia barua ambayo inaweza kuchukuwa wiki kama si mwezi kufika uko ulikoituma na ikitokea mmeonana mtaani basi ni lawama za hapa na pale, kosa ni kutotembeleana.

Hali hii siku hizi imeondoaka nikawa najiuliza, kulikoni mambo haya, kumepita maswahibu gani hapa, siku hizi kutembeleana imekuwa mpaka msiba au harusi ndio utawaona ndugu na jamaa wakipiga hodi nyumbani kwako. Baada ya kutafakari kwa kina nikagundua kuwa haya maendeleo ya simu na mitandao ndio imepelekea mpaka ndugu na jamaa kutotembeleana tena.

Maana ukitaka tu kujuwa hali ya nduguyo au jamaa yako basi vidole vinafanyakazi, na teba siku hizi simu za smatifone ndio kabisa, maana hata ukitaka kumuona nduguyo wee unabofya tu, mara whatsapp, viber au skype, mwaonana hivi na kuzungumza. Hali hii kwa kiasi Fulani nahisi kama imeondoa uhalisia wa binadamu kutembeleana na hata mapenzi kidogo yamepungua, maana kama mtu una hamu ya nduguyo au jamaa yako, huna haja tena ya kufunga safari na kwenda kumsalimia, we wabofya tu, bofyoo, mnayamaliza kwenye simu.

Tena hizi simu za kisasa ukifanya mchezo kwa wale walioko kwenye ndoa unaweza kugombana na mwenziwako, maana hakuna tena yale mahaba mkikaa mmekaribiana, maana kila mtu yupo bize akibofya na kubofyoa, mara wasapu mara vaiba, mara skaipu, akichukuwa umbea wa uku akipeleka uku, wa kule akipelekea kule, bize kutwa kucha.

Maendeleo ni mazuri lakini maendeleo yanapokuja na tukayavamia kiasi cha kuondoa utu wetu, basi maendeleo hayo yatakuwa yanaturudisha nyuma kiutamaduni na hata kiitikadi, maana zamani kabla ya haya mambo ya video kuingia na kuonyesha vilamu za mauwaji, ujambazi na laana za kila aina, watu tulikuwa tukilala usingizi, lakini tangia haya mambo ya Filamu za video kuzagaa sana mitaani na vijana wetu kuiga kila jambo walionao, uko mitaani kumekuwa uwanja wa vita, usingizi umepotea, ndio utakuta mtu anajenga nyumba kama gereza, milango nondo madirisha nondo, gate la chuma, mbwa na mlinzi juu, na bado akilala anaweweseka kuibiwa.

Sasa zimeingia hizi TV kwa ving’amuzi, hapo ndio kabisaa tena ukijumlisha na hizi playstation na xbox vijana wetu hata kutoka kwenda kucheza mpira viwanjani imekuwa hawaendi tena, kila kitu hapo hapo.

Mbaya zaidi kuna huyu mtaalam wa mambo yote, anajulikana sana kama intaneti akishirikiana na nduguye gugo dot komu, hapo ndio balaa, maana uko kuna kila kitu, watu siku hizi wamekuwa wajuwaji, maana hata kama kitu hakijui, mbio anabofya gugo anachukuwa makapi, chenga, mchele safi na pumba vyote anakusanya na kuvikumbatia. Tena wamekuwa mahodari sana, utawaambia nini na gugo yupo mwenye kujuwa kila kitu?

Haya maendeleo si mabaya kama utachunga mustakabari wetu na kuweka hishima kwa kila mtu tunayewasiliana naye, tukirisha utamaduni wa kusoma vitabu na kuwaenzi walimu wetu na waliotuzidi umri, hakika tutakuwa tumetunza hishma yetu mila na utamaduni wetu.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!