27 March 2013Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe mwishoni mwa wiki iliyopita (Jumamosi, 23 na Jumapili, 24 Machi 2013) alitembelea baadhi ya shughuli za miradi mbalimbali  zinayofanywa na Watanzania waishio Leicester and Northampton kwa lengo la kufahamu mafanikio na changamoto zao.

Akisindikizwa na Afisa wa Ubalozi, Bw. Amos Msanjila, Balozi alipenda kufahamu  nini mahitaji ya Watanzania hao ili kuweza kujenga mkakati muafaka wa kuwatia moyo na kuwashirikisha wananchi hao kujenga nchi.Akiwa Leicester alipata fursa ya kutembelea kituo cha redio ya jamii ya mji huo na kufanyiwa mahojiano ya moja kwa moja kwa Kiswahili na Mtangazaji wa redio hiyo, Bw. Omar Hussein. Redio hiyo inasikika moja kwa moja katika maeneo yote  ya Leicestershire na vitongoji vyake.
Aidha Balozi Kallaghe alitembelea kiwanda kidogo  cha usindikaji wa vyakula na viungo kinachomilikiwa na mfanyabiashara mwenye asili ya Tanzania cha Jalpur Millers. Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho Bw. Deepen J. Pau alimwambia Balozi kwamba Kampuni yao ina mipango ya kuwekeza zaidi Tanzania.


Baadae Mheshimiwa alitembelea kituo cha kuratibu usafirishaji wa mizigo mbalimbali kwa makontena kwenda nchi za Afrika Mashariki na hasa Tanzania. Pamoja na kuonyeshwa shughuli mbalimbali zinazofanyika hapo, Balozi alipata pia fursa ya kuzungumza na wajasiliamali Bw. Abdul  Nasser Hamed wa Zanzibar Driving School na Mussa Issa Mussa wa BMA Store and Shipping Agency.


Alipata pia  fursa ya kutembelea mgahawa wa  biriyani wa Maalim Hamis na kukutana na mpishi huyo maarufu kabla ya kukutana na Watanzania wachache, hasa viongozi wa Jumuiya ya Watanzania ya Leicester.


Siku ya Jumapili Balozi alitembelea Jambo Hair Salon na baadae kukutana na viongozi wa watanzania wachache kwenye Mgahawa wa Kass’s Grill unaomilikiwa na kijana wa kitanzania Kasongo Mohamed. Pamoja na kupata chakula cha mchana kwenye mgahawa huo, Mheshimiwa alifanya na mazungumzo na watanzania hao na kusisitiza umuhimu wa mshikamano na moyo wa kuunga mkono biashara za watanzania wenzao.

Mheshimiwa ataendelea kutembelea miji mbalimbali hapa Uingereza na kujionea shughuli zinazofanywa na Watanzania kila atakapopata fursa ya kufanya hivyo.   
  
Reactions:

0 comments:

Post a Comment

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!